Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K. Mongella, amewaongoza wakazi wa mkoa wa Arusha, kuadhimisha Siku ya UKIMWI DUNIANI 2023, Desemba 1, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mazingira Bora wilaya ya Karatu.
Mheshimiwa Mongella, amewataka wananchi kushiriki katika kutokomeza UKIMWI, kwa kuhakikisha kila mmoja anajilinda na kumlinda mweingine kwa afya na maendeleo ya jamii na Taifa.
Amesema kuwa, maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani, yanaikumbusha dunia kujihadhari na ugonjwa huo pamoja na kuunga mkono juhudi za mashujaa, watalamu, ndugu, jamaa na marafiki, walipoteza maisha kutokana na Ugonjwa wa UKIMWI.
Ameongeza kuwa, siku hii muhimu imkumbushe kila mtu kupima na kujua afya yake na pale anapogundulika ameathirika, apate ushauri na kuanza kutumia dawa za kufubaza UKIMWI
Ameweka wazi kuwa, Serikali ya awamu ya sita imewekeza fedha nyingi, kwenye sekta ya Afya hususani katika utoaji na upatikanaji wa huduma za Virusi vya UKIMWI na UKIMWI kwa kutoa bure, Dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI, ili waathirika waweze kupata muda wa kuishi na kufanya kazi kwa maendeleo yao binafsi na taifa lao.
Mratibu wa UKIMWI, Magonjwa ya ngono na Homa ya Ini mkoa wa Arusha, Dkt. Haika Ernest Mhando, amesema kuwa, kulingana na tafiti ya mwaka 2017 - 2016, hali ya maambukizi kwa mkoa wa Arusha ni asilimia 1.9, na kwa kipindi cha Januari mpaka Novemba 2023, jumla ya watu 1,253,000, walijitokeza kupima maambukizi ya VVU.
Amefafanua kuwa, kati ya hao, watu 3,586 walikutwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI sawa na 2.8 % , wanaume ni 2.4% na wanawake ni 2.9%, huku wote wanaendelea kupata huduma katika vituo mbalimbali vya afya ndani ya mkoa wa Arusha.
Hata hivyo wana Konga Karatu, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwahudumia wathirika kwa kuwapa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI, dawa ambazo zinasaidia waathirika kuishi muda mrefu na kujitegemea kwa kufanya kazi za kulijenga Taifa na kujipatia kipato kwa maendeleo ya Taifa.
"Mimi nilizaliwa na Virusi vya UKIMWI, lakini uwepo wa dawa za kufubaza virusi, zimenisaidia ninaishi mpaka leo kwa amani, nikitekeleza kazi zangu kama watu wengine" Amesema Emmanuel Fransisca
Awali, Katika Maadhimisho hayo Mkuu wa mkoa huyo, ametembelea mabanda ya maonesho ya afya, wajasiriamali wadogo, na TAKUKURU, yaliyohimiza upimaji wa afya, Ushauri Nasaha na matumizi ya Dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI kwa maendeleo ya jamii na Taifa.
Kauli Mbiu : Jamii Iongoze, Kutokomeza UKIMWI.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.