Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella ameagiza wakala wa Nishati ya umeme Vijijini (REA) kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi waliopewa zabuni za kusambaza umeme huo na kuwalisha mipango kazi yao kwa wakati kabla kupewa idhini ya kuanza kuweka miundombinu ya umeme kwa wananchi.
Aidha serikali imetoa sh.bilioni 44.4 kwaajili ya ukamilishaji wa umeme kwenye vijiji 103 vilivyopo Mkoa wa Arusha lakini bado kunaonekana kusuasua kwa uwekaji umeme huo kwa wakandarasi waliopewa zabuni hizo.
RC Mongella, ametoa agizo hilo wakati alipofanya kikao kazi na wajumbe wa bodi na watendaji wake kutoka REA waliofika Jijini Arusha kujionea hali halisi ya uunganishwaji wa umeme katika vijiji 103 vya Mkoa wa Arusha.
RC Mongella alibaini wakandarasi waliopewa zabuni za kusambaza umeme vijijini kusuasua kutokana na kutokuwa na fedha za kuanza miradi na kutegemea kulipwa fedha na REA na kupelekea kuwasha umeme kweye kijiji kimoja huku vijiji 43 vikishindwa kufikiwa na umeme huo maeneo ya wilaya za Ngorongoro,Meru pamoja na Arusha Dc
Alisema kukosekana kwa umeme huo wa REA awamu ya III mzunguuko wa pili kwa wananchi kunaleta lawana kwa wananchi dhidi ya serikali kumbe wakandarasi ndio wanaokwamisha kazi kwa wakati.
"Yani nauliza wewe mkandarasi unapewa kazi ya kusambaza umeme unawasha umeme kijiji kimoja huku vijiji vingine 43 vikiwa havina umeme,sasa hii sitaikubali na naomba REA mlichukue jambo hili kwa udharura zaidi ili muangalie mkandarasi asiye na viwango akae pembeni maana anakwamisha juhudi za serikali za kupeleka maendeleo kwa wananchi".
"Haiwezekani serikali itoe hela halafu nyie wakandarasi mnashindwa kumaliza miradi kwa wakati.
Ameitaka REA kuhakikisha wakandarasi wanaleta mipango yao kazi kabla ya kupewa miradi ili wajue wanauwezo gani,maana sababu wanazosema hazina mashiko kama hawana vifaa waseme au ni mtaji".
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya REA,Mhandisi,Styden Rwebangila alisema bodi hiyo imefika Mkoani Arusha na kuwaita wakandarasi wanaosuasua kukamilisha miradi ya umeme Ili kubaini kwanini wanashindwa kukamilisha usambazaji huo wa umeme kwa wakati ilihali walipewa kazi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupitia REA kupeleka umeme vijijini .
Alisema maendeleo ya usambazaji wa umeme huo sio mzuri hivyo waseme tatizo ni nini na kama bodi tujue la kufanya sababu muda wao wa kazi waliopewa unaisha mwezi wa sita na mwingine unaisha mwezi ujao hatua zichukuliwa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.