Na Elinipa Lupembe.
Wawekezaji wa waTaasisi ya Vietnam Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Prof. Salmin Ibrahim Salmin, wamefika kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha na kufanya mazungumzo mafupi na Mkuu wa mkoa huo, Mhe. John V.K.Mongella, leo tarehe 20 Desemba 2023.
Akizungumza kwa niaba ya wawekezaji hao, Prof. Salmin amesema kuwa, wawekezaji hao wanaojihusisha na miradi ya Kilimo, viwanda vya kusindika mazao, madini pamoja na kusafirisha bidhaa zitakazozalishwa nje ya nchi, wako mkoani Arusha kwa ajili ya kutafuta eneo la kuwekeza mradi huo.
Amesema kuwa mradi huo, unaotarajiwa kuanza mapema Januari 2024 huku wakia na matarajio ya kushirikiana na wakulima wazawa kwa kuwapa pembejeo za kilimo, mikopo ya vifaa vya kilimo, ujenzi wa nyumba nafuu pamoja na kuwajengea uwezo wa kilimo cha kisasa.
Awali Mhe. Mongella amewakaribisha mkoani humo kwa ajili ya kufanya uwekezaji kama yalivyo malengo yao na kuwaeleza nia thabiti ya Serikali ya awamu ya sita inayongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuweka mazingira ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya Nchi pamoja na kuwahikikishia mazingira rafiki ya kufanyia shughuli zao.
Amebainisha kuwa, uwekezaji huo ni muhimu kwa mkoa wa Arusha, na zaidi utaleta manufaa kwa taifa kupitia kodi pamoja na kuwanufaisha wananchi kwa kupata ajira na wengine kupata soko la malighafi zao watakazozalisha kutokana na kilimo.
Aidha, amewaahidi ushirikiano mkubwa wawapo Arusha kwa kuhakikisha uwekezaji watakaoufanya, utaleta faida kwa pande zote mbili, kwa nchi na wawekezaji pia.
Hata hivyo, wawekezaji hao, wameishukuru serikali ya Tanzania, mkuu wa mkoa wa Arusha kwa kuwapa fursa ya kuwekeza na kuwakaribisha mkoani Arusha na kuahidi kushirikiana na watanzania kufanya shughuli za uzalishaji kwa manufaa ya wote.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.