"Ndugu viongozi na wafanyakazi, kuhusu hoja ya kuboresha kanuni ya ukokotoaji wa mafao (kikokotoo) serikali imepokea ushauri uliotolewa hata hivyo ni muhimu kuzingatia kwamba uendeshaji na usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni suala la sayansi ya watakwimu bima, hivyo tunategemea wataalamu wetu watushauri kuhusu suala hili la uhimilivu na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii, Mheshimiwa Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan).
Tunawahakikishia wafanyakazi kwamba hakuna mtu angependa kuona watu waliotimikia nchi hii wakiathirika kwa kukosa kiinua mgongo stahiki au pension zao, kutokana na hali hiyo ndio maana serikali iliposhauriwa na wataalamu husika serikali ya awamu ya sita (6) ilichukua uamuzi mkubwa wa kulipa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii kiasi cha shilingi trilioni 2.147 hatua ambayo kwa kiasi kikubwa imeimarisha mifuko hiyo" -Dkt. Mpango
"Lakini vilevile tumeendelea kuimarisha utendaji kwenye mifuko hiyo na kupunguza ucheleweshaji wa malipo ya wastaafu, kwa hiyo kwa kifupi serikali imepokea hoja kuhusu kubadilisha kikokotoo kwa ajili ya kuifanyia uchambuzi zaidi maana kama ilivyosemwa kwenye risala wafanyakazi hawaridhishwi na kanuni hizo, na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake ni wasikivu sana" -Dkt. Mpango
"Hata hivyo, uamuzi wa kubadilisha kikokotoo ni lazima utokane na tathmini ya kina ya kisayansi ya watakwimu bima, ni matumaini ya serikali kwamba TUCTA itashiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kuwasilisha maoni yatakayoimarisha zaidi mifuko" -Dkt. Mpango
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amezungumza hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani (Mei mosi) iliyofanyika kitaifa jijini Arusha
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.