Serikali ya awamu ya sita imekiri kutambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na madereva wa Serikali katika kukuza uchumi wa Taifa la Tanzania kwa kuzingatia majukumu yao na umuhimu wake.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa, wakati akifungua Kongamano la tatu la Madereva wa Serikali, linalofanyika mkoani Arusha kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha, Agosti 20,2024.
Kada hii ya udereva ni muhimu kwa Serikali kutokana na huduma wanayoitoa kwa viongozi na Maafisa wa Serikali, kada ambayo injini inayochochea maendeleo ya Taifa la Tanzania ikiwa inagusa jamii moja kwa moja na kuwasisitiza kufanya kazi kwa weledi.
"Madereva wa Serikali fanyeni kazi kwa uadilifu, simamieni maadili ya kazi kwa kuzingatia mahusiano mazuri mahala pa kazi, nidhamu kazini ni suala la msingi sana, kuheshimu alama za barabarani kwa kuzingatia usalama wa barabarani unaanza na wewe, lindeni usalama wa abiria na waenda kwa miguu pamoja na usalama wa vifaa vinavyotumika"Amesema Waziri Mkuu
Hata hivyo, Waziri Mkuu, ameweka wazi kuwa, Serikali itaendelea kuboresha miundo ya kiutumishi kwa madereva ili kuboresha maslahi yao, huku ikiwa imefanya mapitio ya miundo hiyo na kufanikiwa kubadilisha miundo ya madereva 1, 600 pamoja na kutoa vibali vya ajira mpya, jambo ambalo limechangia idadi ya madereva kuongezeka.
Ameongeza kuwa, Kongomano hilo likatoe hamasa ya madereva kwenda kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia taratibu maadili ya udereva, kanuni, taratibu za utumishi wa Umma pamoja na miongozo ya Serikali, hali itakayoipa heshima kada ya udereva kuwa kama kada nyingine.
Tunafahamu malengo ya chama ni kuikuza kitaaluma na kada ya udereva, kukemea matendo maovu yanasababisha kuiondolea heshima kazi ya serikali, kuongeza umakini na uzingatiaji wa usalama barabarani unakuwa ni kipaumbele cha kila dereva.
"Niwapongeze kwa kuwa Chama hiki kinaendelea kukua na kuwa na sauti kubwa ndani ya Serikali, viongozi wa chama na wizara simamieni madereva kukutana kila mwaka ili kujadili mafanikio na changamoto zao, kukutana kwao kunatoa fursa ya kuboresha utendaji kazi kwa kubadilishana uzoefu, kujadili mambo muhimu kada hii na kuziwasilisha Serikalini ili zifanyiwe kazi" Amesema Mhe. Majaliwa
Hata hivyo Waziri Mkuu, amefurahishwa na kauli mbiu ya Dereva Jitambue, Timiza Wajibu wako, Usalama Barabarani Unaanza na wewe" ambayo imebeba ujumbe muhimu na wa kipekee hasa kwa madereva na maslahi ya taifa, kwa kutambua na ufahamu majukumu yao, dhamana ya kuwahudumia viongozi na wananchi na umuhimu wa kutekeleza majukumu na kuzingatia sheria na usalama wa barabarani.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.