Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe.John V.K Mongela ametoa salamu za pole kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na Watanzania wote, kwa niaba ya Serikali kufuatia vifo vya watu 25, vilivyotokana na ajali ya gari iliyotokea jana jioni Februari 24, 2024 eneo la Ngaramtoni wilaya ya Arumeru.
Mhe. Mongella ametoa pole wa ndugu jamaa na marafiki waliokusanyika nje ya jengo la kuhifadhia maiti, kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, wakisubiri maelekezo ya Serikali kuhusu msiba huo mapema leo Februari 25, 2024.
Amesema kuwa, Serikali inatoa shilingi milioni moja kwa kila marehemu, ikiwa ni ubani kwa ajili ya kugharamia shughuli za mazishi pamoja na kutoa jeneza kwa familia zitakazohitaji kulingana na imani za dini zao.
Amewasilisha salamu za pole kutoka kwa viongozi wakuu wa nchi, wakiongozwa na Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye yupo safarini Namibia kushiriki mazishi ya kiongozi wa nchi hiyo.
"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa wafiwa wote, na ameagiza tushirikiane kwa pamoja kama wanaArusha na kama watanzania, kuwafariji wenzetu, na kwamba Serikali iko pamoja na wafiwa wote, na ameagiza Serikali kutoa ubani wa shilingi milioni moja kwa kila marehemu kwa ajili ya kusaidia shughuli za mazishi pamoja na kugharamia matibabu ya majeruhi wote" Amesema Mhe.Mongella.
Aidha, Mhe. Mongella ameweka wazi kuwa, msiba huo ni wa watanzania wote na Serikali imetoa kibali kwa ndugu na familia za merehemu kuanza kuchukua miili kwa ajili ya mazishi na tayari baadhi yao wameanza kuchukua miili hiyo.
Hata hivyo Mhe. Mongella amebainisha kuwa Serikali imeandaa utaratibu wa kugharamia matibabu ya majeruhi 21 waliotokana na ajali hiyo, na wanaoendelea na matibabu tangu jana, madaktari na wahudumu wa afya wanapambana kuhakikisha wanarejea afya zao.
Kufuatia ajali hiyo jumla ya majeruhi 21 wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye Hospitali mbalimbali huku majeruhi 11 wakiwa wamelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Arusha Mount Meru.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamshna Msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11 jioni, ambapo Lori lenye namba za usajili KAS 943, likiwa na Tela lenye namba TF67, likitokea Namanga, lilipoteza mwelekeo na kugonga magari matatu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.