Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, jumla ya Hospitali za wilaya 129 zimejengwa kote nchini Tanzania katika jitihada za kuboresha huduma za afya nchini.
Akizindua Jengo la Wagonjwa wa Nje katika hospitali ya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha leo septemba 19, 2024, Waziri Mchengerwa pia amesema Rais Samia amefanikiwa kukarabati hospitali kongwe zaidi ya 28 huku Monduli ikiwa miongoni mwa wanufaika wa ukarabati huo.
"Jengo hili ambalo mmenipa heshima ya kuja kulizindua nataka niwathibitishie kuwa kiwango hiki cha fedha kilichoingia Monduli kimekwenda nchi nzima katika hospitali kongwe zilizojengwa miaka ya 1960 na 1970." ameongeza kusema Mhe. Waziri Mchengerwa.
Jengo hilo lililozinduliwa leo Alhamisi na Mhe. Mchengerwa aliyeambatana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda lina thamani ya zaidi ya milioni 460 likiwa na uwezo wa kuhudumiwa wagonjwa takribani laki mbili ambapo Waziri Mchengerwa pia ametumia nafasi hiyo kukemea uzembe kwa wataalamu wa afya, suala ambalo limekuwa likisababisha vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.