Na Prisca Libaga - Arusha
Serikali imeanza kufanya matengenezo ya kwenye daraja kubwa la Tenganyeti na miundombinu ya kingo za barabara katika eneo la wilaya Longido, mkoa wa Arusha, daraja linalounganisha nchi za Tanzania na Kenya, kufuatia uharibifu uliotokana na mvua zilizonyesha kwa zaidi ya saa saba, usiku wa kuamkia Novemba 25 huku zikihatarisha kukata mawasiliano ya barabara kati nchi hizo, kupitia mpaka wa Namanga.
Serikali imeanza jitihada za kulinusuru daraja hilo, lililopo kilometa chache kabla ya kuingia katika Kituo Jumuishi cha Forodha (OSBP- One Stop Border Post) cha Tanzania na Kenya cha Namanga, ambacho kimekuwa na shughuli nyingi za kuingiza na kutoa bidhaa kati ya nchi zote mbili.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania - TANROADS, Mhandisi, Mohammed Besta, amefika katika Daraja hilo na kutoa maelekezo kwa TANROADS Mkoa wa Arusha, kuendelea na jitihada za kulifanyia marekebisho daraja hilo, ili lisiendelee kuharibika zaidi.
Hata hivyo, Mhandisi Besta amewatoa hofu, Watanzania, kuwa barabara zote nchini zipo salama na wamejipanga kukaniliana na uharibifu wowote utakaojitokeza kwa kipindi hiki cha Mvua.
"Kazi inayoendelea hapa, ni muendelezo wa kukabiliana na matukio ya dharura kwa kipindi chote cha mvua, ni watake Mameneja wa mikoa yote kuwa tayari kukabiliana na uharibifu wa barabara utakaotokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini"Ameweka wazi Mhandisi Besta.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe ametaja kuendelea na mikakati ya usanifu wa daraja hilo pamoja na udhibiti wa mikondo ya maji, ili kunusuru daraja hilo kuendelea kuharibika.
Mkuu wa Wilaya ya Longido Marco Ng'umbi ameeleza kuwa, barabara hiyo ni umuhimu kwa wananchi na uchumi wa nchi zote mbili na Afrika Masharikia, hasa katika usafirishaji wa malighafi na bidhaa za kibiashara, ikiwemo mazao ya chakula.
"Sisi Mpaka wa Namanga ndio lango kuu la biashara, ikitokewa mawasiliano ya barabara yamekata, kutatokea athari kuwa, za kijamii na kiuchumi, kipekee tunaishukuru Serikali na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Kuijali Longido kwa kuboresha miundombinu ya barabara" Amesema Mhe. Ng'umbi
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.