SERIKALI YAANZA KUTOA VITAMBULISHO VYA KISASA KWA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO
Uzinduzi Kabambe wafanyika Arusha!
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imezindua rasmi ugawaji wa vitambulisho vya kidijitali kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe.Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wafanyabiashara hao na wananchi wa jijini Arusha wakati akizindua vitambulisho hivyo leo Oktoba 17, 2024, amebainisha kuwa vitambulisho vitakuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara ndogondogo kuwainua kiuchumi.
Amesema Serikali kwa vipindi tofauti imeendelea kushughulikia changamoto za wafanyabiashara ndogondogo na kwa kutambua juhudi hizo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendeleza juhudi hizo kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia na ukuaji wa uchumi jumuishi.
Waziri Dkt. Gwajima amezitaja baadhi ya juhudi hizo ni pamoja na ujenzi wa ofisi za wafanyabiashara ndogondogo na kuwapanga kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa na Serikali ambapo hadi sasa mikoa kumi na mbili (12) imekamilisha ujenzi wa ofisi hizo.
Ametaja pia uboreshaji wa miundombinu unaotekelezwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, uratibu wa utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara ndogondogo ambapo Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali zimeendelea na jitihada za kuwaendeleza kiuchumi ikiwemo mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri na mikopo kutoka Baraza la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi na Wizara ya Viwanda na Biashara.
"Kwa upande wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeingia mkataba na Benki ya NMB wenye thamani ya Shillingi Bilioni 18.5 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara hao. Vilevile Wizara itaendelea kutumia mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) kuwezesha wanawake wajasiliamali." amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda akizungumza katika tukio hilo, ametoa wito kwa wafanyabiashara ndogondogo kutumia fursa hiyo ya pekee kwao ili kujinufaisha zaidi kiuchumi huku akiwahimiza wananchi wote kushirikiana kutokomeza vitendo vya ukatili kwa kutoa taarifa za ukatili.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.