Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko, amewaagiza Mawaziri na Makatibu Wakuu, kuhakikisha Taasisi zote za Umma, zinatumia mfumo wa wa kielekroniki wa Manunuzi ya Umma - NeST katika manunuzi yote ya Serikali ili kuongeza tija na ufanisi.
Mhe.Dkt.Biteko ametoa maagizo kwa niaba ya Mhe. Rais Dkt. Samia, Suluhu wakati akifungua Jukwa la 16 la Ununuzi wa Umma, kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimatifa Arusha, Septemba 09,2024.
“Ninawaelekeza pia Mawaziri na Makatibu Wakuu wote kuhakikisha kuwa Taasisi zilizochi chini ya Wizara zenu, kuhakikisha zinautumia mfumo wa NeST, ninashangazwa kusikia, pamoja na jitihada za Serikali kuwa na mfumo wa NeST, kuna baadhi ya Taasisi za Umma hazitumii mfumo huo katika shughuli za ununuzi"Amesisitiza Dkt.Biteko
Aidha, amemuelekeza Waziri wa Fedha kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine, kuhakikisha wote waliopewa jukumu la kuongoza Taasisi za Umma kutumia mfumo wa NeST, ili kujihakikishia usahihi na udhibiti wa fedha za Serikali.
Ameongeza kuwa, kwa Tanzania mfumo huo, umeleta manufaa makubwa kwa kupunguza gharama za matumizi ya karatasi, kuongezeka kwa kasi ya ununuzi,kupungua kwa makosa katika ununuzi na kuboresha utoaji huduma kwa wazabuni na wananchi.
“Nimefurahi kusikia mfumo huu pia umeongeza uwazi, uwajibikaji na kuleta thamani ya fedha katika ununuzi ni wazi kuwa mfumo huu utaleta faida nyingine nyingi ikiwemo kuimarisha utawala bora,kuongeza wigo wa ununuzi na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa".Ameongeza.
Aidha alisema Serikali imeendelea kudhibiti matumizi ya fedha zinazopelekwa kwenye kila fungu kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mifumo ya kielektroniki ili kuleta tija na ufanisi unaostahili katika utekelezaji wa Bajeti ya fungu husika.
Hata hivyo amekiri kuwa, Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kisheria katika ununuzi wa umma ambayo yalianza Mwaka 2001 kwa kutungwa kwa sheria ya kwanza ya Ununuzi wa Umma, baada ya changamoto kadhaa, zilizosababisha mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2004, na kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.