Serikali ya awamu ya sita, kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na ofisi ya Rais - TAMISEMI pamoja na Wadau mbalimbali, imejipanga kuweka Mbinu Jumuishi za Ushirikishwaji wa Jamii kuhusu m-mama ili kuongeza uelewa kwa jamii wa mfumo huo.
Katika kutekeleza adhma hiyo, watumishi wa Sekta ya Afya na wadau wengine wamefanya kikao cha kujadili Mbinu Jumuishi za Ushirikishwaji wa Jamii kuhusu m-mama kilichofanyika kwenye ukumbi wa Olasit Garden, Mkoani Arusha Julai 010,2024.
Akizungumza kwenye Kikao hicho, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, James Mhinu, amesema kuwa lengo la kikako hicho ni kuwajengea uwezo washiriki kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuhusu mfumo huo pamoja na kutengeneza mpango kazi wa utekelezaji wa kazi hiyo.
Mhinu ameeleza kuwa kikao hicho ni muhimu kwaajili ya kukuza ushirikiano wa karibu kati ya wadau mbalimbali na kujenga msingi imara wa kuendeleza na kukuza matumizi ya teknolojia ya m-mama kwa manufaa ya jamii na maendeleo endelevu.
Aidha, Mfumo huo ulianzishwa kwa lengo la kupunguza vifo waj watoto wachanga na wajawazito wakati wa kujifungua nchini, kwa kuimarisha mfumo wa usafiri wa dharura kwa gharama nafuu kwa kutumia teknolojia, sambamba na ushirikishwaji wa jamii kwenye kutoa huduma ya usafiri mbadala pale inapohitajika.
Hata hivyo, mfumo huo umetengenezwa kuwa endelevu na nafuu kwa jamii na wananchi kupata fursa ya kupiga namba ya simu 115 bure ili kupata msaada wa haraka huku rufaa 90,000 zikiwa zimesafirishwa na zaidi vituo vya afya 7,600 vilichanganuliwa, sambamba na Serikali kuanzisha dawati la msaada mtandaoni kwa Mikoa ili kuripoti matatizo yoyote kuhusu m-mama.
Inakadiriwa kuwa takribani akina mama 2,370,000 wanapata ujauzito kwa mwaka ambapo Akina mama zaidi ya 300,000 sawa na asilimia 15% wanapata changamoto zitokanazo na uzazi, na katika hawa ni asilimia 6 tu sawa na takribani akina mama 45,000 watakaohitaji usafiria wa dharura na Akinamama wanaojifungulia kwenye Vituo vya Kutolea huduma za Afya ni sawa na asilimia 83.
Awali, Mfumo huo ulizinduliwa rasmi kwa awamu III ukijumui mikoa yote nchini huku awamu ya kwanza ikiwa mkoa wa Shinyanga na awamu ya pili mikoa ya Mara, Arusha, Singida, Katavi, Iringa na Mtwara
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.