Na Elinipa Lupembe.
Kufuatia mkakati wa Serikali ya awamu ya sita ya viongozi kukutana na wanachi kusikiliza kero zao na kuweka mipango ya kuzitatua, jambo hilo limetekezeka na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella kwa kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Enguserosambu na kusikiliza kero zao.
Katika mkutano huo Diwani wa kata ya Enguserosambu Mhe. Wiliam Oseitain Paremiria, amewasilisha changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo ikiwa ni pamoja na wananchi kukamatwa na Uhamiaji kwa kutuhumiwa kuwa sio raia wa Tanzania kutokana na kutokuwa na Vitambulisho vya Taifa(NIDA)
Ameiomba serikali kuwapa vitambulisho vya Taifa wakazi hao, ili kutatua changamoto hiyo ya kukamatwa inayoleta usumbufu mkubwa kwa wananchi na kuongeza kuwa wakiwa na vitambulisho vya Taifa, itaondoa udanganyifu kwa watu wasio raia ambao huingia nchini kinyemela.
"Vijiji vyetu viko mpakani, kuna muingiliano wa kijamii na kiuchumi na nchi jirani ya Kenya, Uhamiaji wanashindwa kutofautisha yupi ni raia hivyo ni vema wananchi wakapata vitambulisho vya Taifa ili kuondoa usumbufu kwa raia wetu wema"Amesema Mhe. Diwani
Akijibu hoja hizo, Mhe. Mongella amefafanua kuwa, Serikal imetatua changamoto zilizokuwa zinaikabili Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa- NIDA na sasa tayari wameanza kutoa vitambulisho kwa watu ambao tayari walikwisha jiandikisha
Niwatoe wasiwasi, muda si mrefu NIDA wataanza kutoa vitambulisho kwenye wilaya na kuongeza kuwa mkoa wa Arusha umepokea zaidi ya vitambulisho 490 na vitagawanywa kwa watu ambao walikwisha jiandikisha mara vitakapowasili wilayani kwa utaratibu mzuri tofauti na hapo awali.
Hata hivyo amewataka wananchi hao kutii sheria na kujikita zaidi katika kufanyakazi halali za uzalishaji mali ili kujiingizia kipato huku wakitambua namna serikali inavyopambana ili wananchi wake wapate huduma bora kwa kuwafikia katika maeneo yao.
"Nimefurahi sana kukutana na wananchi wa hapa,kwa niaba ya Mama Samia, ninawapongeza kwa kujitoa kwenu kufanya shughuli za maendeleo, mmeanza ujenzi wa shule ya sekondari, niahidi serikali haitawaacha peke yenu, nitakuja kuwaunga mkono ili shule hiyo ikamilike na watoto wa Enguserosambu wasome hapa hapa kwa kuwa kila kata inatakiwa kuwa na shule ya sekondari" Amesisitiza Mhe. Mongella
Mhe, Mongella amewagiza TARURA kufanya usanifu kwenye barabara ya fupi ya kutoka Waso na kufahamu gharama za ujenzi wa daraja ili kuwarahisishia usafiri wananchi hao, ambao kwa sasa wanatumia barabara waliodai inazunguka mpaka kufika kijijini hapo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.