Shirika lisilo la kiserikali la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika -WiLDAF limetambulisha rasmi mradi wa Wanawake Sasa ambao utatekelezwa mkoani Arusha kwa kipindi cha Miaka mitatu 2024 - 2027.
Akizungumza kwenye kikao kifupi cha kutambulisha mradi huo, kilichofanyika kwenye ofisi ya kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Agosti 21,2024 Mkurugenzi wa shirika hilo, Anna Kulava, amesema kuwa mradi huo wa Wanawake Sasa una lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na maamuzi ili kubadili fikra za kutambua uwezo sawa wa wanaume na wanawake katika uongozi.
katika kipindi hicho mradi utatekelezwa kwenye halmashauri za Jiji la Arusha na Meru, ukifanya kazi ya kuwajengea uwezo wanawake na kuwahamasisha kushiriki kwenye chaguzi kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
"Mradi unalenga kuwafikia angalau wanawake 50 kila halmashauri na kuwajengea uwezo wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika maeneo yao hasa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika mapema mwezi Novemba Mwaka huu" Amesema Anna.
Amesisistiza kuwa, wanawake na vijana wanapaswa kutambua kuwa uongozi ni hatua hivyo kuanza katika nafasi ndogo ndogo za uongozi ambao utamjenga na kudhhirisha kama mtu huyo akishika nafasi kubwa ya uongozi atafanya vizuri zaidi.
“Mradi huu unalenga zaidi kuwafikia na vijana vijana na kuwajengea uwezo wa kutambua kuwa uongozi sio lazima ngazi za juu tu bali hata nafasi ndogo zina umuhimu kwa vijana.” Amesisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Katibu tawala na Afisa Utumishi Mkuu Mkoa wa Arusha Elgin Nkya, amewakaribisha wadau hao mkoani Arusha na kuwaahidi ushirikiano katika kutekeleza mradi huo huku akisisitiza kuwa, kuwatenga wanawake katika nafasi za uongozi ni sababu za kudumaza maendeleo hasa katika nchi za Afrika.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.