Na Elinipa Lupembe
Shule mpya ya msingi Emairete kata ya Monduli Juu, ikiwa umbali wa Km 11 kutoka makao makuu ya wilaya hiyo, shule ambayo imeanza Januari 08, 2024, ikiwa na wanafunzi 457 waliohamishiwa kutoka shule ya msingi Monduli Juu.
Mradi huo, umetekelezwa kwa shilingi milioni 470, fedha kutoka Serikali Kuu kupitia Mradi wa Kuboresha Upatikanaji wa Fursa sawa katika Ujifunzaji Bora kwa Elimu ya Awali na Msingi Tanzania Bara (BOOST), umewaondolea mwendo wanafunzi wa kijiji cha Emairete, waliotembea umbali wa takribani Km 10 kwenda shuleni kila siku.
Wanafunzi hao, wameishukuru Serikali ya awamu ya sita, chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga shule, ambayo wamekiri kuifurahia kutokana na ukweli kwamba, shule waliyosoma awali, ilikuwa mbali na kuwasababisha kutembea umbali mrefu huku wengi wao walikosa masomo kutokana na makorongo kujaa maji, wakati wa msimu wa mvua.
Meleji Meshilo mwanafunzi wa darasa la 7, amekiri kufurahia kuhamishiwa shuleni hapo, shule yenye majengo mazuri na ya kisasa, ikiwa karibu na nyumbani, jambo ambalo limewapunguzia mwendo, tofauti na awali walitembea umbali mrefu.
"Wakati nasoma Monduli Juu, nilikuwa mchelewaji, kila siku nilichelewa shule kutokana na umbali, nilianza kukata tamaa ya kusoma, kwa sasa nimeanza na ari mpya, nitasoma kwa bidii" Ameweka wazi Meleji
Naye Riziki Lesikar (7), amebainisha kuwa, mvua ikinyesha makorongo hujaa maji, na kuwalazimu kushindwa kwenda shule na kukosa vipindi vingi wakati wa msimu wote wa mvua.
"Tunamshukuru sana Rais wetu, Mama Samia, kwa kutujengea shule nzuri, madarasa ni mazuri, walimu wanatufundisha vizuri, mimi na wenzangu tunaahidi kusoma kwa bidii, natamani kufikia ndoto yangu ya kuwa daktari" Amesema Riziki
Hata hivyo, mwalimu Mkuu Msiadizi Mwl. Metui Saruni, ameweka wazi kuwa, shule ina jumla ya wanafunzi 457 darasa la awali mpaka la saba, ambao asilimia 90, wametokea shule ya msingi Monduli Juu.
Ameongeza kuwa licha ya kupunguza msongamano wa wanafunzi shule waliyotokea, pia wamepunguza kutembea umbali mrefu, shule mpya yenye miundombinu ya kisasa, ina mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia kwa walimu na wanafunzi.
Ikumbukwe kuwa, miradi hiyo ya ujenzi wa miundombinu shule za msingi ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, Sura ya tatu Ibara ya 79 kifungu (q)Kukarabati miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na kifungu (C) Kuboresha uratibu na usimamiaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.