Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jaffo, ameiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Longido kuweka mipango thabiti ya kusimamia ujenzi wa kituo cha afya cha Oriendeki na hospitali ya wilaya ya Longido.
Mheshiwa Jaffo ameyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua miradi hiyo katika wilaya ya Longido,mapema wiki hii.
“Sijaridhishwa kabisa na kasi ya ujenzi kwenye wilaya hii,hata fedha zilizoletwa hapa kwenu ni nyingi ukilinganisha na maeneo mengine, sasa inakuwaje nyinyi mmepata fedha nyingi na mmeshindwa kumaliza ujenzi na bado mnataka serikali iwaongezee fedha zaidi?”.
Aidha, mheshimiwa Jaffo amemtaka mkurugenzi wa halmshauri ya Longido Daktari Jumaa Mhina, Mganga Mkuu wa wilaya, afisa manunuzi,muweka hazina wa wilaya na wakuu wa idara kuandika barua za maelezo ya kwanini wameshindwa kumaliza miradi hiyo ijapokuwa serikali ilishatoa fedha za kutosha.
Amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo kwani serikali imeshatoa fedha za kutosha za kumaliza ujenzi huo lakini anashangaa kwanini mpaka sasa miradi hiyo haijakamilika na fedha zimeisha.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Idd Kimanta amesema wameyapokea maelekezo yote ambayo yametolewa na mheshimiwa Jaffo kwa utendaji zaidi.
Mheshimiwa Jafo yupo katika ziara ya siku 2 Mkoani Arusha kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na hospitali za wilaya.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.