Na Elinipa Lupembe.
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wameyakubali maombi ya Nchi ya Somalia, kuwa Mwanachama wa Nchi za Jumuyia hiyo ya Afrika Mashariki na kuifanya Jumuiya hiyo kuwa na Nchi 8, ikiwemo.Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, na Somalia
Maamuzi hayo, yalifanyika kwenye kikao cha Ndani na hatimaye, kuyaweka bayana, wakati wa kuhitimisha, Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), uliofanyika Mkoani Arusha, kwenye viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto Mountain Lodge wilayani Arumeru.
Licha ya kuwa, Rais wa Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud, alihudhuria Mkutano huo wa 23, kwa mara ya kwanza, na Nchi yake kukubaliwa kuwa mwanachama wa Jumuiya hiyo, huku Marais wa Jumuiya hiyo wakipata wasaa wa kumpongeza Rais huyo kwa niaba ya wananchi wa nchi hiyo, kwa kujiunga na kuwa mwanachama wa Umoja huo muhimu kwa manufaa na maendeleo ya wananchi wa nchi hizo.
Naye, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, amempongeza Rais wa Somalia, kwa kujiunga na Jumuiya hiyo pamoja na kushiriki mjadala wa mabadiliko ya tabia Nchi na Usalama wa Chakula, wenye lengo la kujiweka imara katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko hayo bila kutegemea misaada kutoka nje ya Afrika.
"Tumefurahia nchi ya Somalia kujumuika nasi, kwa kuwa sisi ni ndugu moja, tunayo mengi zaidi tunayofanana kuliko tunayotofautiana" Amesema Mhe. Samia
Awali, katika mkutano huo, Rais wa Sudan Mhe. Salva Kiir Mayardit, amekuwa Mwenyekiti wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, baaaya kupokea kijiti kutoka kwa Rais wa Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye, ambaye amemalliza muda wake.
Mara baada ya kuchaguliwa, Mhe. Salva Kiiri, amekabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi, kwa kipindi chote cha kuiongoza Jumuiya hiyo, nafasi ambayo inadumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mkutano huo wa siku mbili, ulihusisha Wakuu wa Nchi za Wananchama wa Jumuiya za Afrika Mashariki, licha ya mambo mengine yaliyojadiliwa, ulijikita katika kujadili kuhusu masuala ya Tabia Nchi na Usalama wa Chakula, ukiwa umebeba Kauli Mbiu ya "Kuharakisha ufufuaji wa uchumi kupitia hatua za hali ya hewa na kuimarisha usalama wa chakula kwa ajili ya kuboresha maisha" (Theme Accelerating Economic Recovery through Climate Action and enhancing Food Security for Improved Livelihoods), ukitanguliwa na vikao vya ndani tarehe 23 Novemba na kumalizika, tarehe 24 Novemba, 2023.
#eastafricacommunity
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.