Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imefanya kikao na balozi wa Singapore nchini Tanzania Douglas Foo na kuelezea fursa za uwekezaji zinazopatikana kwenye hifadhi za Taifa ili kuvutia wawekezaji kuja Nchini na kuwekeza kwenye maeneo hayo.
Kikao hicho kilichojumuisha wajumbe kutoka Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, TAWA na AICC kimefanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Ngorongoro, Jijini Arusha ambapo wamewasilisha vivutio mbalimbali vya uwekezaji kwa Balozi huyo.
Akizungumza wakati akiwasilisha taarifa ya fursa za uwekezaji ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) Mkurugenzi wa kituo hicho Christina Mwakatobe, lisha ya kumkaribisha Balozi huyo kutembelea na kujionea fursa zinazopatikana kituoni hapo, amesema kuwa Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika kuendesha mikutano ya Kimataifa kwa nchi za Afrika ambapo kwa sasa inashika nafasi ya 5 huku akiamini kuwa kulingana na Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, idadi hiyo itaongezeka na hata kufikia nafasi ya tatu bora.
"Katika kipindi cha miaka 3 ya hivi karibuni, tumeshudia ongezeko la wageni wengi ambao pia baada ya kufanya mikutano hupenda kutembelea maeneo ya hifadhi na kujionea vitu mbalimbali vya asili ambavyo nchi yetu imebarikiwa na kisha kurudi kwao". Amesema Mkurugenzi huyo.
Aidha, fursa zingine za uwekezaji zinazopatikana kwenye maeneo ya hifadhi ni pamoja na maeneo ya vivutio vya kupiga picha, uwindaji na maeneo ya kuweka kambi za muda mfupi na muda mrefu.
Hata hivyo, Balozi huyo ameahidi kuendelea kushirikiana na Nchi ya Tanzania sanjari na kueleza watu wa Nchi yake juu ya fursa hizo za kufanya uwekezaji na kukuza Sekta ya Utalii sambamba na kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi, Bishara na Uwekezaji, Frank Mmbando ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wageni wote kuja kujionea vituo vilivyomo ndani ya Mkoa wa Arusha na kufanya uwekezaji utakaosaidia kukuza pato la Taifa na kuwaletea wanachi Maendeleo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.