WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema, Tanzania inaunga mkono uamuzi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) juu ya kuongeza mbinu za uvunaji wa maji, udhibiti wa mafuriko na miundombinu ya kuhifadhi maji hayo ili yatumike wakati wa ukame ama kiangazi kuzuia mafuriko msimu wa mvua nyingi.
“Tanzania inaunga mkono uamuzi huo na inasisitiza Sekretariet ya SADC kuongeza misaada kwa nchi wanachama katika ujenzi wa mabwawa ya kutunza maji ambayo yatatumika katika vipindi vya ukame na kiangazi pamoja na kuzuia mafuriko katika vipindi vya mvua,” amesema.
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumatatu, Mei 20, 2024) wakati akizungumza kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kuhusu athari za mvua za El Nino. Ameshiriki mkutano huo kwa njia ya mitandao kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.
Maamuzi hayo yaliyopendekezwa kwenye kikao cha Mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo yalitaka ziongezwe mbinu za uvunaji wa maji, udhibiti wa mafuriko na miundombinu ya kuhifadhi maji kwa msaada kutoka kwa Sekretarieti ya SADC, Mashirika ya Uendelezaji Mabonde ya Mito (RBOs) na wadau wa maendeleo ili kuongeza nguvu ya kukabiliana na ukame ama mafuriko yanayosababishwa na hali ya hewa kwenye ukanda wa SADC.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa ni kuboresha utendaji wa Usimamizi wa Rasilimali za Maji Jumuishi (IWRM); kufuatilia viwango vya maji na kutekeleza huduma za WASH; kuboresha usimamizi wa maji yanayohusisha nchi zaidi ya moja na ushirikiano wa kimataifa; kuhamasisha uhifadhi wa maji na kukuza matumizi ya maji machafu yaliyotibiwa na maji yaliyochujwa chumvi (desalination).
Akielezea kuhusu ujenzi wa mabwawa ya kutunzia maji ambayo yatatumika katika vipindi vya ukame na kiangazi pamoja na kuzuia mafuriko katika vipindi vya mvua, Waziri Mkuu aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa Serikali ya Tanzania tayari imeandaa Mpango Mkakati wa Ujenzi Malambo 40 Nchini (rain water ponds) kuanzia Novemba 2023 hadi Julai 2024 ambao ni awamu ya kwanza.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.