Mitambo yote iliyokuwa ikitumika katika ujenzi wa barabara chini ya halmashauri ikabidhiwe kwa wakala wa barabara za vijijini na mijini(TARURA).
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo alipokuwa akifunga mkutano wa 40 wa baraza la barabara la mkoa wa Arusha.
“Nawaagiza viongozi wote wa halmashauri kwenda kusimamia makabidhiano ya mitambo yote yakutengeneza barabara iliyokuwa inatumiwa na halmashauri kwenda kwa TARURA kwa kufuata taratibu zote husika.”
Amesema moja ya changamoto wanayokumbana nayo watalaamu kutoka TARURA ni ukosefu wa vitendea kazi hususani mitambo ya barabara ambayo mingi bado imeshikiriwa na halmshauri karibia zote isipokuwa halmashauri ya Jiji la Arusha.
Pia, amezitaka halmashauri zote kuhakikisha zinatenga fedha za kutosha kwa ajili ya uchangiaji wa shughuli za TARURA na kuziwasilisha mapema iwezekanavyo.
Ameitaka TARURA kuhakikisha inafanya kazi zake kwa karibu sana na halmashauri ili kuongeza ufanisi wa kazi zao.
Akitoa taarifa ya hali ya barabara ya mkoa kaimu mratibu wa TARURA injinia Dickson Kanyakole, amesema TARURA imejitaidi sana kuongeza mtandao wa barabara kutoka 3838 hadi 6928.
Amesema pia changamoto nyingine ni upatikanaji wa malighafi za kutengenezea barabara kama vile changalawe na mawe kwani maeneo wanayoyapa yanamilikiwa na vijiji hivyo kupelekea kuwa na wakati mgumu wakuyapata kwa wakati husika.
Kikao cha bodi ya barabara cha mkoa wa Arusha kimekaa kwa mara ya kwanza mwaka huu 2018/2019 ikiwa ni robo mwaka kwa lengo la kufanya tathimini ya utendaji katika mkoa hasa kwenye miundombinu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.