Na. James Mwanamyoto Ofisi ya Rais - Tamisemi
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe amewaelekeza watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha wanafanya vikao kazi kila baada ya wiki mbili ili kuboresha usimamizi wa utoaji wa huduma ya afya msingi nchini.
Dkt. Magembe ametoa maelekezo hayo leo wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kilicholenga kuhimiza uwajibikaji katika eneo la usimamizi wa utolewaji wa huduma za afya msingi nchini.
“Ili kutekeleza kikamilifu majukumu ya idara ya afya, naelekeza kukutana kila baada ya wiki mbili kwa ajili ya kujadili changamoto zinazotukabili, kuanisha shughuli tulizozitekeleza vizuri na kufanya tathmini ya utendaji kazi wetu ili kuwa na ufanisi endelevu wa utekelezaji wa majukumu ya idara yetu,” Dkt. Magembe amesisitiza.
Dkt. Magembe amesema, wananchi wanaotibiwa katika ngazi ya afya ya msingi ni kati ya asilimia 77 hadi 80 hivyo jukumu la Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ni kubwa kwasababu inawahudumia wananchi wengi walio katika mamlaka ya Serikali za Mitaa.
“Tunawafikia wananchi wengi na si tu kwenye eneo la tiba bali ni pamoja utoaji wa huduma za chanjo, uzazi wa mpango, lishe na ustawi wa jamii, hivyo huduma nyingi wananchi wanazipata kupitia ngazi ya afya ya msingi na hii ni kwasababu zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya ndio zipo karibu na wananchi,” Dkt. Magembe amefafanua.
Dkt. Magembe ameongeza kuwa, kwa kuwa sehemu kubwa ya wananchi wanategemea huduma katika ngazi ya afya ya msingi hivyo ni muhimu kwa watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa na ubora unaotakiwa, zinakidhi matarajio ya wananchi na zinapatikana muda wote.
“Ninyi na mimi ndio tumepewa jukumu la kuhakikisha tunasimamia na kuratibu utekelezaji wa afua zote za sekta ya afya, kutekeleza maagizo na maelekezo ya viongozi, kuwasimamia vema watumishi wa sekta ya afya walio katika ngazi ya afya ya msingi ili watoe huduma bora, ikiwa ni pamoja pamoja na kupokea maoni na kero wananchi dhidi ya huduma zinazotolewa,” Dkt. Magembe amehimiza.
Sanjari na hilo, Dkt. Magembe amewataka watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kuwa na mawasiliano ya kila siku na watumishi wa sekta ya afya walio katika ngazi ya msingi ili kutatua changamoto wanazoweza kukabilisana nazo wakati wa kuwahudumia wananchi.
Dkt. Magembe amefanya kikao kazi na watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kazi cha Septemba 17, 2024 kilicholenga kuimarisha usimamizi wa huduma za afya msingi nchini.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.