Chama cha wanawake Mawakala wa Utalii Tanzania (TAWTO) wamekarabati Jengo la Ofisi ya Polisi Masuala ya Jinsia na watoto, Wilaya ya Arusha na Kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella.
Jengo hilo, lililokuwa uchakavu kutokana na kujengwa kwa muda mrefu, lilepambwa kwa michoro inayovutia ya wahanga wanaofanyiwa ukatili kueleza zaidi changamoto wanazokumbana nazo kwenye jamii pamoja na kuwekwa samani za ofisi.
Akikabidhi jengo hilo Jijini Arusha, Mwenyekiti wa TAWTO, Elizabeth Ayo amesema chama hicho kimeona umuhimu wa kukarabati jengo la Dawati hilo, litakalosaidia katika kusimamia na kulinda haki za wanawake na watoto pamoja na watoa huduma ambao ni Jeshi la Polisi.
"Tumeamua kuunga mkono juhudi za Serikali kwa fedha kidogo tuliyojaliwa kama chama ili jamii hususani wanawake na watoto waweze kupata haki kwenye mazingira rafiki kwa wahusika". Amesema.
Akizungumza wakati akikabidhiwa jingo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. JOHN V.K Mongella, amewashukuru wadau hao kwa kujitolea kusadia kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa jamii kupitia Dawati hilo la Jinsia kwani wanafanya mambo makubwa katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakua kupitia sekta ya utalii.
"Hiki mlichofanya Mungu atawalipa sababu kuna watu wanataabika na unyanyasaji ikiwemo ukatili kwa watoto, wanawake na wanaume ambapo sasa ukarabati huu utatoa ari zaidi katika kutafuta suluhu ya changamoto za ukatili ikiwemo kulinda haki za watoto na kinamama".
Hata hivyo Mhe. Mongella ametoa rai kwa wananchi wote kutojihusisha na vitendo vya kikatili kwa makundi yote na kusababisha madhara ya kisaikolojia kwani hatua za kisheria zitaendelea kufuata mkondo wake ili kudhibiti matukio hayo huku akitoa wito kwa wadau wa maendeleo kuiga mfano wa Taasisi hiyo kwa kujitokeza na kutoa michango yao kusaidia jamii.
Akisoma taarifa fupi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ambaye ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Arusha, Ursula Mosha amesema dawati la Jinsia na watoto ni dawati lenye kusaidia jamii kuhusu kupinga unyanyasaji wa kijinsia wanaofanyiwa wanawake, watoto na wanaume ambapo Awali dawati hilo lilianzishwa mwaka 2010 kwa kuhudumia jamii na kushauri dhidi ya ukatili.
Amesema kuwa dawati hilo linatoa huduma ya ushauri kwa wanandoa ikiwemo elimu na makuzi, kuunganisha familia zilizotengana pamoja, ushauri wa usiri kwa wahanga wa ukatili katika Dawati la Jinsia la Huduma kwa Pamoja lililopo Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru ikiwemo utoaji wa elimu kwa jamii.
Pia Alishukuru TAWTO kwa kusaidia ukarabati wa jengo hilo lililokuwa chakavu kwa kupewa meza tano za kisasa,viti kumi na mabenchi matatu ikiwemo marekebisho ya upakaji rangi,paa sakafu ikiwemo michoro ya kuhamasisha watoto wanapofika dawati kutoa changamoto zao za ukatili.
"Tunalengo la kuwa na jengo huru ili kutoa uhuru kwa wahanga wanaofanyiwa ukatili na pia michoro itakapokamilika tunawaomba wadau wajitokeze zaidi kuchangia dawati hilo tunawashukuru sana TAWTO kwaukarabati huu"
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.