"Nendeni mkasimamie haki bila kupindisha sheria ili kuepusha kuumiza wasiostahili na kuwafurahisha wenye pesa zao".
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifungua mkutano wa 27 wa wanasheria wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jijini Arusha.
Kupindishwa kwa sheria kumesababisha watu wengi kutotendewa haki na kufungwa kwa makosa ambayo siyo yao na wale waliotakiwa kuhukumiwa kuachwa huru.
Aidha,amewataka wanasheria hao kuangalia njia sahihi zitakazosaidia nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweza kuingia katika ushirikiano zaidi na kuufanya umoja huo kuwa wenye tija na nguvu.
Amesisitiza zaidi, katika kubadilishana uzoefu kwa wanachama ili kujengeana uzoezi utakaosaidia kufanya kazi nzuri hata za nje ya jumuiya hiyo.
Nae,Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Geofrey Mizengo Pinda amewataka wanasheria wa Tanzania kujiunga kwa wingi katika chama cha wanasheria wa Afrika Mashariki ili waweze kupata nafasi ya kufahamika na kupata fursa za nje ya nchi zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amewataka wanasheria hao kutumia fursa hiyo ya Kikao kutembelea mbuga mbalimbali za wanyama ili wajionee wanayama waliopo katika Mbuga za nchi.
Mkutano huo wa wanasheria wa Afrika Mashariki umejumuisha nchi za Tanzania bara na visiwani,Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, DRC Congo na takribani wajumbe zaidi ya 100 wameweza kuhudhuria.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.