"Sensa haina kikwazo cha kiimani, hivyo kila mmoja atoe ushirikiano na kujitokeza kuhesabiwa siku ya Agosti 23."
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella alipokuwa akizungumza na viongozi wa dini, kisiasa, Kimila, viongozi wa wabodaboda, machinga na wenyeulemavu katika kikao cha kuhamasisha sensa.
Amesema ili zoezi la sensa liweze kufanikiwa hatuna budi tuendelee kushirikiana kuhamasisha kama tunavyoshirikiana kwenye mambo mengine ya maendeleo katika Mkoa wetu.
Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Mkoa wa Arusha Hashimu Msemwa amesema, kwakua Rais Mama Samia anatafuta njia njingi za kuleta maendeleo katika nchi hasa kutoka nje ya nchi hivyo wao wapo tayari kumuunga mkono katika kujitokeza kuhesabiwa ili iwe rahisi kwa yeye kujua kiasi cha maendeleo yanayoitajika.
Nae, mwenyekiti wa machinga Arusha Amina Njoka amesema wao wanaendelea kuhamasishana kwenye masoko yako.
Pia, Katibu wa walemavu Mkoa wa Arusha Yunus Urasa amesema, wanafurai kwa zoezi la sensa kuwa shirikishi kwao, na wataweza kupata idadi halisi ya walemavu katika Mkoa na nchi kwa ujumla.
Ameziomba Jamii zenye walemavu watoe ushirikiano katika zoezi la sensa ili walemavu wote waweze kuhesabiwa.
Naibu mwenyekiti kamati ya amani Mkoa wa Arusha Hussein Gulamu amewataka viongozi wa dini waendelee kuhamasisha kwenye nyumba zao za ibada ili waumini wajitokeze kuhesabiwa.
Askofu Israel Masa kutoka Jumuiya ya maridhiano amesema, wao wamekuwa wakihamasisha kila wanapokutana na waumini wao na kwa njia ya simu.
Kiongozi wa Kimila Lwaigwanani Isack Meijo Olekisongo amesema, Taifa lisipofanya sensa ni sawa na kutembea gizani,hivyo wao wataendelea kuhamasisha jamii zao wahesabiwe.
Kikao cha viongozi wa taasisi mbalimbali kimefanyika katika ngazi ya Mkoa kama mwendelezo wa kampeni ya Mhe. Mongella katika kuhamasisha sensa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.