Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bwana Missaile Musa amesema amefurahishwa na kabila la Wasonjo wanavyo fanya kazi kwa ushirikiano katika kujiletea maendeleo.
Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Ngorongoro.
" Natamani makabila mengine ya Mkoa huu yangeiga kama Wasonjo wanavyo fanya ya kuanzisha miradi ya maendeleo kwa nguvu zao".
Hii inatia Moyo hata kwa Serikali kuweka nguvu zaidi katika miradi hiyo kwani ikiachwa ikafa inakuwa ni hasara.
Amelitaka kabila hilo la Wasonjo waendelee kujitoa kwa hali na mali na serikali haitawaacha,itawaunga Mkono kwa kila mradi watakaouwanzisha.
Aidha, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuongeza kasi ya kumaliza ujenzi wa miradi ili iweze kukamilika kwa wakati na kuleta manufaa kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Dkt. Jumaa Muhina amesema wamepokea maelekezo yaliyotolewa na Katibu Tawala na watayafanyia kazi kwa haraka zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sale Musa Radia amesema mafanikio ya kuanzishwa kwa miradi mbalimbali kumetokana na mshikamano uliopo kwa rika mbalimbali za Jamii hiyo ya Kisonjo.
Kila rika katika Jamii hiyo imeweka utaratibu wa kuanzisha mradi ambao utaacha kumbukumbu kwa vizazi vingi ili na wao waweze kuiga kwa waliotangulia.
Jamii hiyo huwa inaangalia changamoto zilizopo katika Jamii na kutatua kwa kuanzisha mradi husika, kama vile wamejenga Chuo Cha Ufundi VETA, Kituo cha Afya na sasa wanaendelea na ujenzi wa shule ya Sekondari.
Katibu Tawala Missaile amefanya ziara ya siku moja katika Wilaya hiyo na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa chuo cha uwalimu, jengo la ofisi ya halmashauri,chuo cha VETA, zahanati ya Samunge, Kituo cha Afya Sale, Hospitali ya Wilaya na ujenzi wa shule mpya.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.