KAMATI YA SIASA MKOA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO YA BILIONI 1.6 MERU.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha Ndugu Zelothe Steven Zelothe amesema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya na elimu katika Halmashauri ya Meru.
Zelothe ameyasema hayo wakati kamati ya siasa Mkoa wa Arusha ikikagua utekelezaji wa ilani ya CCM kwa Mwaka 2022/2023 kwenye miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Serikali.
Zelothe amesema kupitia ziara hiyo kamati ya siasa imeona thamani ya fedha kwenye miradi hiyo.
Aidha,ameishauri halmashauri kuwashirikisha wananchi wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hali kadhalika, halmashauri imetakiwa kuhakikisha wanatatua changamoto za wananchi sambamba na utoaji wa taarifa za miradi ili kuwajengea uwelewa.
Nae, Katibu wa CCM Mkoa Musa Matoroka, amewataka wataalamu wa halmashauri kukagua miradi hiyo mara kwa mara ili kuongeza nguvu katika usimamizi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru Mhe. Jeremia Kishili, amesema halmshauri hiyo itaendelea kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili fedha zaidi zipatikane katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na wananchi waweze kupata wanachokihitaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema, serikali itaendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo ili fedha zinazotolewa na serikali zipate thamani yake kwenye miradi hiyo na kuweza kusogeza huduma bora zaidi kwa wananchi.
Ziara ya Kamati ya siasa ya Mkoa imejikita katika ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa wananchi ili kuhakikisha ilani ya CCM imetekelezwa vizuri.
Halmshauri ya Meru imekusanya jumla ya fedha bilioni 3.7 kutoka kwenye mapato ya ndani na zaidi ya milioni 935 zilipelekwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo huku bilioni 1.6 ni fedha zilizotolewa na serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya na elimu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.