Wanawake Wilayani Longido wametakiwa kutumia ardhi katika kuzalisha ili walete maendeleo katika familia zao na jamii kwa ujumla.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe, Iddi Kimanta alipokuwa akigawa hati miliki za kimila kwa wanawake 233 kutoka Tarafa ya Engarenaibor katika Kijiji cha Mairowa Wilayani Longido.
“Niwapongeze sana wababa kwa kuridhia kutoa ardhi kwa ajili ya wamama, hiki ni kitendo cha ushujaa na faida ni kwa familia yote”.
Amesema Wilaya ya Longido imeweka historia mpya kwa kuwaruhusu wanawake kumiliki ardhi kitu ambacho hakikuwepo tokea mwanzo kutokana na mila na desturi za jamii ya Kimasai.
Kimanta amesema kupatikana kwa hati miliki hizo kuna toa fursa kwa wanawake kuweza kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji, ikiwemo kupata mikopo kutoka katika Halmashauri na Mabenki ili waweze kuwekeza zaidi katika miradi.
Amesisitiza kuwa kwa wanawake kumiliki ardhi kutasaidia kupunguza migogoro ya ardhi ambayo mingi ilikuwa inasababishwa na wamama wengi katika familia kushindwa kuwa na haki yakumiliki ardhi.
Aidha, Kimanta amesema serikali itashirikiana na Baraza la wanawake wafungaji (PWC) kuhakikisha wanawake katika jamii ya kimasai wanamiliki ardhi na kuwa na maamuzi ya kifamilia na hata jamii yao pia.
Nae katibu Tawala Wilaya ya Longido bwana Kamana Simba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Frank Mwausumbe amewataka wakinamama hao kutozifungia hati miliki hizo katika makabati, bali wakazitumie katika uzalishaji kwa maendeleo ya familia zao na jamii yote.
Mbunge wa jimbo la Longido Mhe. Steven Kiluswa amewataka wakinamama hao waliopewa hati miliki za ardhi kutoenda kuanzisha mafarakano katika familia zao.
Amewahasa pindi wanapotaka kuuza ardhi wawashirikishe waume zao au Watoto, wasiuze kimya kimya kwani ndio chanzo cha migogoro mingi ya ardhi katika jamii hiyo ya Kimasai.
Mashaka Mtatilo ni afisa ardhi kutoka halmashauri ya Longido amesema, mpaka sasa jumla ya vijiji 38 vimeshapimwa ardhi kati ya vijiji 49 na zoezi la upimaji linaendelea katika vijiji hivyo vilivyosalia.
Baraza la wanawake wafugaji limekuwa likitoa mchango mkubwa sana katika kuwainua wanawake wa jamii yakifugaji katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Uchumi hasa katika wilaya hiyo ya Longido.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.