Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt Athumani Kihamia amesema wilaya ya Longido ni moja ya wilaya iliyopewa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa shule shikizi kutokana na Jiografia ya eneo hilo,na kutoa wito kwa wasimamizi wa ujenzi kutofanya ubadhirifu wa fedha hizo.
Dkt Kihamia alisema wilaya hiyo imepewa sh billion 1 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa 50 maeneo mbalimbali katika wilaya,fedha hizi ni za moto msijaribu kuzitumia kinyume na kile kilichoagizwa.
Akizungumzia hali ya miradi inavyotekelezwa ,alisema pamoja na kuwa wilaya hiyo upatikanaji wa Nyenzo(Material) kwa ajili ya ujenzi ni changamoto lakini viongozi wamejitahidi kusimamia tofauti na maeneo mengine ambayo malighafi zinapatikana kwa haraka.
" Mmejitahidi na mpo kwenye hatua nzuri,lakini haimaanishi kuwa mmeshamaliza kazi, bado tutarudi kukagua na wataendelea kuja watu kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kukagua miradi hii ikiwemo TAKUKURU"Alisema Dkt Kihamia.
Katika hatua nyingine,aliwahasa wazazi kuwapeleka watoto shule na kuachana na desturi ya kuwachungisha mifugo,kwani serikali inatambua haki ya elimu kwa mtoto ndio maana Rais Samia ametoa fedha za ujenzi wa Madarasa hayo na kuwasogezea huduma karibu watoto wasiendelee kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Jacob Laizer Mkazi wa Kata ya Orbomba Tarafa ya Longido akizungumza kwa niaba ya wananchi alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa kuleta fedha za miradi ya elimu na kudai kuwa shule nyingi wilayani humo zenye ufaulu duni wa watoto ni kutokana na umbali mrefu wa kwenda shule.
Alisema,uwepo wa shule hizo karibu na jamii kutasaidia kupunguza kuzorota kwa elimu kwa watoto wa jamii ya kifugaji,kwani Uvivu wa kutembea zaidi ya kilomita 10_25 kufuata elimu utapungua na watoto watasoma kwa raha.
" Hata hivyo watoto wetu walipokua wakitembea umbali mrefu kufuata elimu kwenye shule mama za msingi walikua wakikutana na wanyama wakali hali hiyo pia ilikua ikiwatia hofu na kukata tamaa ya kuendelea na masomo na kupeleka utoro sugu wa wanafunzi" alidai Laizer.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya Nurudin Babu katika ziara yake aliwasisitiza jamii hiyo kutumia majengo hayo pindi yatakapo kamilika kwa kuhakikisha watoto wanakwenda shule ili yasibaki kama Ghofu na nyumba ya wadudu Kama vile Buibui.
Aidha aliwataka jamii kujiongeza kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika maeneo yaliyojengwa shule shikizi sambamba na Madarasa hayo ili watoto watakapoanza kusoma wapate huduma ya vyoo na kuepuka kujisaidia maeneo yasiyorasmi Mfano vichakani.
" Naomba acheni tabia ya kuwakeketa watoto wakike pamoja na ndoa za utotoni" aliomba Babu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Longido Stephen Ulaya alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa maji na matofali,lakini wamejipanga kukabiliana nalo na ifikapo Desemba 15 Madarasa hayo yatakua yamekamilika.
Ikumbukwe kuwa fedha hizi ni fedha za Mpango wa serikali ya Tanzania wa kuinua Uchumi kwa kutumia mkopo wa fedha wa Sh. Trillion 1.3 uliotolewa na shirika la fedha Duniani (IMF) na kukabiliana na ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO 19).
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.