Na.Mwandishi wetu, Arusha
Waziri wa Habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, Mhe. Nape Nauye ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini kutoa majina katika Mitaa na barabara ambayo yatakuwa na kumbukumbu ya historia ya nchi kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha akiwa katika oparesheni maalumu ya kukagua zoezi nzima la anwani za makazi.
Majina hayo yatasaidia kutunza historia ya nchi kama kutumia majina ya viongozi mbalimbali au wabunifu.
Amesema kwa Mkoa wa Arusha anwani za makazi zitasaidia sana utalii kwani watalii wataweza kutumia mfumo huo kufika mahali wanapotaka kwa urahisi zaidi.
Mhe. Nape amesisitiza umuhimu wa kuwa na anwani za makazi ni urahisi wa kuhudumiwa, kuwasiliana na hata kukutana kistaarabu.
Aidha, amewaomba viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao walione kama nila kwao ili kuendelea kumuunga Mkono Rais wetu.
Pia, ameupongeza Mkoa wa Arusha kwa kuendelea kufanya vizuri zoezi hilo japokuwa mazingira ya Mkoa niya kusambaa lakini bado zoezi linakwenda vizuri.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amemwakikishia Waziri kuwa zoezi hilo litakamilika ifikapo Aprili 30,2022 kabla ya ile tarehe ya Kitaifa Mei 30.
Amesema Mkoa unaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili walichukulie zoezi hili kama la kwao.
Nae, Katibu Mkuu wa Wizara ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari Dkt. Jim Yonazi ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kubuni kalakana inayosaidia kupunguza gharama za utengenezaji wa mabomba.
Amesema wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano ili kuwezesha zoezi hilo kukamilika vizuri na kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe.Said Mtanda amesema Wilaya yake imeshatambua jumla ya nyumba 122,000 na zoezi zima limeshafikia asilimia 78.
Akitoa taarifa ya Mkoa, Katibu Tawala msaidizi Mipango na uratibu bwana Said Mabiye amesema zoezi la kuweka anwani za makazi lilizinduliwa rasmi mnamo Februari 12,2022 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Amesema zoezi hilo hadi sasa linatumia mfumo wa kijitali unaonesha kiwango cha uwekaji wa Anwani za makazi katika Mkoa mzima.
Mhe. Nape amefanya Operasheni ya anwani za Makazi kwa siku moja Mkoani Arusha ambapo amefanya kikao na viongozi mbalimbali wa Mkoa na Jiji la Arusha na pia aliweza kagua uwekaji wa vibao katika Barabara na Mitaa na amekagua kalakana inayotengeneza mabomba ya vibao vya majina katika Jiji la Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.