Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassm Majaliwa amewataka wafanyabiashara wadogo (Machinga) kukaa katika meza zao walizopangiwa ili waweze kutambulika na kupata mikopo kirahisi.
Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na Machinga wa soko la Kilombero alipofanya ziara ya kukagua masoko ya Machinga katika Jiji la Arusha.
" Acheni kukimbia meza zenu, zitawasaidia kutambulika na kupata mikopo kwa urahisi kwa mabenki".
Mhe. Majaliwa amesema Serikali itaendelea kusimamia maboresho ya masoko hayo ili yawe katika hali inayotakiwa.
Aidha, ameitaka halmashauri ya Jiji la Arusha kuendelea kuboresha miundombinu ya masoko yote ya Machinga kwani Serikali imetoa bilioni 1.5 kwa ajili hiyo.
Lengo la Serikali nikuona wamachinga wanakua na kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Amewataka mgambo kutotumia nguvu katika kusimamia wamachinga bali watumie weredi na maarifa kwenye kazi zao za ulinzi.
Nae, Waziri wa TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa amesema, ataendelea kusimamia maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia ya kuhakikisha masoko ya Machinga yanakuwa na miundombinu rafiki.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amesema, Mkoa umeweza kusimamia uwanzishaji wa saccoss ya Machinga ambayo itawasaidia kupata mikopo ya kukuza mitaji yao.
Mhe. Kassim Majaliwa amefanya ziara ya kukagua masoko ya Machinga ya Mbauda, Kilombero na Machame kwa lengo la kujionea hali ya masoko ilivyo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.