Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa TEHEMA kubuni mbinu mbalimbali za kukuza uchumi wa nchi.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha 5 cha TEHAMA Mkoani Arusha katika kituo cha mikutano (AICC).
"Teknolojia ya kijitali ndio inayoongoza ulimwenguni kwa sasa kwani mambo mengi yanaendeshwa kijitali na kuongeza kasi ya maendeleo".
Hata nchi yetu inaweza kufikia hatua hiyo kwani tayari Serikali imewekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha TEHAMA inakuza uchumi wetu.
Pia,Serikali itahakikisha teknolojia hii inawafikia wananchi hata wa Vijijini kwani hadi kufikia 2024 Kilomita 15,000 za Mkongo wa Taifa zitakuwa zimefikiwa kwa gharama ya zaidi ya Bilioni 170.
Aidha, ameitaka Tume ya TEHAMA kusajili wataalamu wa sekta hiyo wa kutosha ili kufikia malengo ya kuwa nao 5000 ifikapo 2025.
Pia, ameitaka Wizara ya Habari, teknolojia ya mawasiliano na habari kushirikiana na sekta binafsi ili kukuza ufanisi zaidi na kusimamia upanuzi wa Mkongo wa Taifa ili huduma ufike hadi katika miji ya Halmashauri zote.
Wizara ishirikiane na Wizara ya Afya katika kutoa taarifa mbalimbali kijitali hasa za ugonjwa wa UVIKO 19, pia katika kutoa elimu juu ya sensa ya watu na makazi itakayofanyika 2022.
Amesisitiza zaidi kwa Wizara kushirikiana na Wizara ya mambo ya ndani katika kuongeza ulinzi na usalama wa miji kwa kufunga kamera katika Mitaa mbalimbali.
Nae, Waziri wa Habari, teknolojia ya mawasiliano na habari Dkt.Ashatu Kijaji amesema Wizara yake imejipanga kuhakikisha TEHAMA inakuwa ndio nguzo kubwa ya uchumi wa Taifa ili kuleta maendeleo.
Wizara imejipanga kuibia vijana wenye ujuzi wa TEHEMA ili kuwaendeleza na kuwasaidia kukuza utalaamu wao huku tukiibua fursa za kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amesema Dunia ya sasa inategemea sana teknolojia ya kijitali katika mambo mbalimbali hivyo ni fursa kubwa kwa watanzania kuichangamkia.
Mkutano wa 5 TEHAMA umefanyika Jiji Arusha chini ya wizira ya Habari, teknolojia ya mawasiliano na habari na kwa mwaka 2022 mkutano huo unatarajiwa kufanyika Zanzibar.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.