Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amezitaka kamati za ulinzi wa mwanamke na mtoto ngazi ya Wilaya kwenda katika ngazi za chini za Mitaa, vitongoji na Vijiji kutoa elimu ya namna ya kukomesha vitendo vya ukali wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Maelekezo hayo yametolewa alipokuwa akifungua kikao cha kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto ngazi ya Mkoa, Jijini Arusha.
Amewataka viongozi wote katika Mkoa kwa ngazi zote kushirikiana kukomesha vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwani havikubariki katika Mkoa wa Arusha na havita fumbiwa macho.
Aidha, amesisitiza zaidi kuundwa kwa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika ngazi za Vijiji, Vitongoji na Mitaa ili viongozi wa ngazi hizo waweze kudhibiti matukio hayo ya ukatili katika maeneo yao.
Pia, amelitaka dawati la jinsia likasimamie kesi hizo za ukatili wa kijinsia ili zipatiwe hukumu kwa mujibu wa sheria na bila kumuonea mtu yoyote.
Nae, Afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Arusha Bi Erena Mateu amesema Mkoa wa Arusha umeshika nafasi ya 3 kati ya Mikoa 7 iliyoongoza katika kuwa na matendo mengi ya ukatili wa kijinsia.
Amesema Mikoa uliyoongoza ni Iringa na Manyara na Mkoa wa Dar es Salaam ukishika nafasi ya 4,ukifuatiwa na Mkoa wa Shinyanga,Kagera na Dodoma.
Afisa ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha bwana Denis Mgiye amesema katika mwaka 2020/2021 jumla ya matukio yaliyolipotiwa ni 4,705 katika ofisi za Polisi, Vituo vya Afya na ofisi ya ustawi wa Jamii.
Amesema mashauri 304 sawa na 6.4% ya mashauri yote ndio yamefikishwa mahakama na mashauri 77 yalitolewa hukumu na watuhumiwa 11 wamehukumiwa.
Kikao cha Kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto kimefanyika katika Mkoa wa Arusha ikiwa ni maagizo yaliyotolewa na Waziri wa TAMISEMI Mhe.Ummy Mwalimu mnamo Julai 2, 2021 kwa lengo la kuona ni namna gani kamati hizi zinaweza kuweka mikakati yakuondoa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.