Wadau watakiwa kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii yetu.
Akifungua kikao cha wadau wa watoto na wanawake wa mkoa wa Arusha,mwenyekiti wa kikao hicho Richard Kwitega, amesema bado jamii inatakiwa kupata elimu zaidi juu ya ukatili huu.
Amesema kati ya mwaka 2017/2018 jumla ya watu 1,437 walifanyiwa ukatili wa kijinsia katika Mkoa wetu wa Arusha, ambapo wahanga wakubwa ni wanawake na watoto na hawa ni wale waliofika maeneo ya huduma kama vile polisi, Vituo vya Afya na Ustawi wa jamii.
Kwitega amesema kuna uwezekano mkubwa idadi hii ikaongezeka kwani si kila mtu anaetendewa ukatili huu wa kijinsia anafika kutoa taarifa katika vituo husika, wapo wanaoficha kwa kuogopa aibu katika jamii zao.
Aidha,amesema kuna madhara makubwa sana yanayotokana na ukatili huo,ikiwemo kushindwa kujishughulisha na shughuli za kiuchumi na hivyo kupelekea kushuka kwa pato ghafi la Taifa.
Akitoa shukrani kwa kuwakutanisha wadau na serikali Mkurugenzi wa Railway Children Afrika Musa Mgata, amesema kukutana kwao kumewapa nguvu zaidi ya kuendelea kushirikiana na serikali kwa karibu zaidi ili kutokomeza ukatili wa kinjinsia kwa wanawake na watoto.
Kikao cha wadau wa watoto na wanawake kwa mkoa wa Arusha kimefanyika kwa lengo la kupitia Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) na kuona ni kwa jinsi gani wadau wanaweza kuisaidia Serikali kwa kutambua majukumu yao.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.