Vijana watakiwa kuhakikisha wanarudisha mikopo yote waliyokopeshwa kwenye vikundi vyao ili kusaidia kukuza mfuko wa Wazira na kutoa fursa ya vikundi vingine kukopeshwa.
Akitoa maelekezo hayo Mkurugenzi wa idara ya vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,ajira,vijana na watu wenye ulemavu, bwana James Kajugusi alipokuwa akitembelea vikundi mbalimbali vya vijana katika halmashauri ya Meru.
Amesema Wizara kupitia mfuko wake wa maendeleo ya vijana ulitoa kiasi cha fedha Milioni 103 kwa halmashauri ya Meru kwa lengo la kukopesha vikundi mbalimbali vya vijana vinavyofanya shughuli za maendeleo na ukuzaji wa uchumi.
“Nashangwazwa sana na taarifa hii ya vikundi vingi vya vijana kupata fedha za serikali lakini wameshindwa kurejesha na hata Saccoss ya vijana Meru ambayo ndio inasimamia fedha hizo imeshindwa kuvifuatilia vikundi hivi ili virejeshe mikopo hii”.
Amesisitiza zaidi juu ya fursa mbalimbali zinazotolewa na Wizara kupitia idara ya vijana mbali na mikopo kuwa ni fursa za kuongeza ujuzi kwa vijana wabunifu ambao hawajasomea na fursa za mafunzo mbalimbli kwa vijana.
Akielezea changamoto zinazosababisha vikundi vya vijana kushindwa kurejesha mikopo Mkurugenzu Mtendaji wa Halmashauri ya Meru bwana Emmanuel Mkongo, amesema vijana wengi hawaaminiani kwenye vikundi vyao na hiyo kupelekea vingi kuvunjika au wanavikundi kukimbia na mikopo hiyo.
Pia, amesema kuna hali ya siasa kuingilia ufuatiliaji wa fedha hizi za mikopo na hivyo kufanya mazingira ya urejeshaji kuwa magumu zaidi na baadhi ya vikundi vya vijana kuingia kwenye siasa hizo.
Aidha, amesema mbali na changamoto hizo bado halmashauri yake kushirikiana na maafisa husika wanaendelea kuhakikisha fedha zote zilitolewa na Wizara na halmashauri zinarejeshwa ili kutoa nafasi ya vikundi vingine kunufaika pia.
Nae mwenyekiti wa kikundi cha Old is Gold Arts group bwana Samola Mloe, amesema mikopo ya vijana inayotolewa na Wizara imesaidia sana kikundi chao kukua na mafunzo waliyopewa na halmashauri yamewasaidia pia kupata masoko kupitia mitandao ya kijamii nje ya nchi.
Bwana Kajugusi yupo katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Arusha kwa lengo la kutembelea vikundi mbalimbali vya vijana na kukagua miradi ya maendeleo inayofanywa na vikundi hivyo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.