Vijana wa Rika katika kabila la Batemi wametakiwa kuwa waadilifu hususani katika shughuli zao wanazofanya katika jamii yao ili kuweza kuleta maendeleo, umoja na mshikamano.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Hassan Kimanta,alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika chuo cha ufundi cha VETA katika kata ya Samunge wilayani Ngorongoro.
Amesema nguvu kubwa iliyooneshwa na rika la vijana la Erumarshari katika kujenga chuo hicho ni mfano wa kuigwa na vijana wengine katika kuleta maendeleo ya jamii zao.
Mwenyekiti wa Rika la Erumarshari bwana Sakanda Gaima amesema,lengo kubwa la kujenga chuo hicho katika Kijiji chao lilikuwa ni kuisaidia jamii hiyo kuondokana na ujinga.
Vile vile amesema chuo hicho kitasaidia kutoa nafasi ya kujiendeleza kimasomo kwa wale wanafunzi ambao hawatafaulu kupangiwa shule za sekondari, watajiendeleze kupitia chuo hicho.
Bwana Gaima amesema, rika la Erumarshari lina jumla ya vijana 419 ambao ndio wameshiriki katika kujenga chuo hicho kwa nguvu zao wenyewe ikiwemo kuchangia fedha kiasi cha milioni 300 na nguvu kazi kutoka kwa vijana hao.
Wameishukuru pia serikali kwa kuwaunga mkono katika ujenzi huo kwani kiasi cha fedha bilioni 1.5 zilitolewa na serikali ili kusaidia ujenzi wa chuo hicho.
Amesema ni utaratibu wa vijana wanapoingia katika jukumu lijulikanalo kama Rika ka tika jamii hiyo kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo rika la kwanza lilijenga kituo cha afya,rika la pili limejenga chuo cha ufundi na rika la tatu limejenga madarasa ya shule ya sekondari.
Vijana wa rika katika kata ya Samunge wanaojulikana kama Erumarshari wamewakabidhi rasmi majukumu ya rika kwa kundi jipya la vijana lijulikanalo kama Erumisidai baada ya kumaliza muda wake wa usimamizi wa maswala ya ulinzi na usalama na maendeleo katika jamii hiyo ya Batemi wilayani Ngorongoro.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.