Mapema leo Machi 26, 2025 vijana zaidi ya 1000 wa Mkoa wa Arusha wamejitokeza kwa katika ofisi za mkoa kwa ajili ya usahili wa kuwania nafasi za ufadhili wa masomo nchini India kufuatia tangazo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, aliyesema kuwa serikali ya India imetoa ufadhili wa masomo kwa vijana 1,000 wa Arusha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa usahili huo, Mhe. Makonda amebainisha kuwa ufadhili huo utahusisha programu na fani zaidi ya 250, ufadhili huo ukisimamiwa na Serikali ya India kupitia kwa Balozi wake nchini Tanzania, Mhe. Bishwadip Dey.
Mhe. Makonda ameeleza kuwa fursa hiyo imetokana na juhudi kubwa alizozifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha uhusiano na mzuri na Mataifa Mengine ambazo zimepelekea nchi kama India kutoa fursa hizo kwa vijana wa Kitanzania.
"Hii ni fursa adhimu kwa vijana wa Arusha kupata elimu bora nje ya nchi, hususan nchini India, ambayo inajulikana kwa ubora wa elimu yake katika nyanja mbalimbali," amesema Mhe. Makonda.
Hata hivyo Mhe. Makonda ameendelea kusisitiza umuhimu wa vijana kujitokeza na kutumia fursa hizi ili kuleta maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine ya ushirikiano huo, Serikali ya India imetoa ufadhili kwa Wajasiriamali 50 wa Arusha kusomea kozi ya Upishi nchini India. Lengo ni kuwawezesha kujifunza mapishi ya vyakula vya Kihindi na tamaduni mbalimbali za taifa hilo, ili kuboresha huduma kwa watalii wa Kihindi wanaotembelea Tanzania.
Kwa upande wao, vijana waliojitokeza katika usahili huo wameelezea furaha yao kwa fursa hii adhimu, wakisema kuwa ni hatua kubwa kwao katika kufikia malengo yao ya kielimu na kimaendeleo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.