Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametangaza kuwa jumla ya Vijiji 12, 333, mitaa 4,269 na Vitongoji 64, 274 vitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Jijini Arusha leo Jumatatu Septemba 16, 2024 kwenye Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mchengerwa amewaambia wanahabari kuwa kwenye orodha hiyo kumejumuishwa maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa tangazo la serikali ambayo pia yalihusisha Tarafa ya Ngorongoro mkoani Arusha.
"Matangazo haya yanajumuisha maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa Tangazo la serikali namba 673 na 674 ambayo yalihusisha pia Tarafa ya Ngorongoro. Lengo la hatua hii ni kuhakilisha kuwa maeneo haya yanapata uwakilishi mzuri kiutawala pamoja na huduma za kijamii na kiuchumi zinazowiana na mahitaji ya wananchi." Amesema Mhe. Waziri.
Akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, Mhe. Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi huo katika kuunda serikali ya wananchi kidemokrasia ikiwa ni pamoja na kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la mpigakura kwa mustakabali wa maendeleo na kuendeleza juhudi za serikali katika kujitafutia maendeleo endelevu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.