Askofu wa Kanisa la Kilutheri Tanzania KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati Mchungaji Godson Abel Mollel na Sheikh wa Mkoa wa Arusha Shaaban Juma Abdallah wamewaongoza wananchi wa Arusha kwenye sala na dua maalum ya kuwaombea maelfu ya wananchi wanaoendelea kupatiwa matibabu kwenye Kambi maalum ya matibabu inayoendelea Mkoani Arusha.
Viongozi hao wa dini wameambatana na viongozi wengine wa madhehebu mbalimbali kwenye viwanja vya Michezo vya Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid leo Juni 27, 2024, huku pia wakimuombea Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili Mungu ampe maono zaidi na nguvu katika kuwatumikia watanzania.
Viongozi hao pia katika dua na sala zao wamemtakia kheri Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda wakimtaja kama Kiongozi mwenye kutanguliza maslahi ya wananchi mbele na mwenye kiu ya kutaka kuwa mtatuzi wa changamoto na kero mbalimbali za Wananchi wa Mkoa wa Arusha.
Viongozi hao wa dini pia wamewaombea baraka watu wote waliofanikisha kambi hii ya siku saba ya matibabu ya kibingwa inayoendelea Mkoani Arusha, wakiomba Huruma ya Mungu pia katika kuwaponya watu wote wenye kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.