Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella amewashauri viongozi wa madhehebu ya Kikristo kuwahimiza waumini wao kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua Kongamano la viongozi wa Dini kwa madhehebu ya Kikristo, Jijini Arusha.
Bila maendeleo waumini hawawezi kutulia na kumuomba muumba wao kwani watakuwa na msongo wa mawazo mengi.
Amesisitiza zaidi kuwa waumini wakifanya kazi kwa bidii na kujiletea maendeleo watakuwa wameleta maendeleo katika Mkoa mzima na nchi kwa ujumla.
Anaamini maendeleo yanaletwa na mtu mmoja mmoja na sio kundi la watu na kufananisha na Imani ya wokovu kuwa ipo kwa mtu mmoja mmoja nasio kundi la watu.
Amesema waumini wakiwa na uchungu wa kutafuta maendeleo yao itawasaidia kuwa na utulivu na kuweza kufuata Sheria na taratibu za Kanisa na hata nchi pia.
Aidha, amewashauri viongozi hao wa madhehebu ya Kikristo wawe na uwezo wa kujua mambo kwa haraka, hii itawasaidia kwendana na wakati na mafundisho yao kuwafikia watu wengi.
Akitoa neno la shukrani mwenyekiti wa umoja wa madhehebu ya Kikristo Kanda ya Kaskazini Askofu Dkt. Stanley Hotay, amesema viongozi hao wapo tayari kushirikiana na Serikali katika nyanja mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kongamano hilo la viongozi wa madhehebu ya Kikristo nchini limeandaliwa kwa ushirikiano na Joyce Meyer Ministry ya nchini Marekani.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.