Viongozi wa mila na desturi nchini wametakiwa kuhakikisha wanadumisha mila na desturi za makabila yao kama wamaasai wanavyoendeleza hasa kwa vijana.
Yamesemwa hayo na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkta. Harrison Mwakyembe, alipokuwa akizungumza na viongozi wa koo za maa na rika za Marya jijini Arusha.
“Nafurahishwa sana na kabila hili la Maasai linavyoenzi na kuthamini mila na desturi zao hivyo basi rai yangu kwa viongozi wa makabila mengine kutumia ujuzi na maarifa waliyonayo kurithisha mila na desturi zao kwa vizazi vilivyopo”.
Amesema hali ya utandawazi kwa sasa inachangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa mila na desturi zetu kwani vijana wengi wanakimbilia kuiga mambo ya utandawazi na kusahau mila na desturi zao.
Tusipochukua hatua leo yakuwajengea hari yakupenda mila na desturi zetu tutawapoteza wote kwani wengi watazamia kwenye mambo ya usasa zaidi.
Amewahasa kulinda amani katika nchi yetu kwani serikali ipo pamoja nao na itaendelea kushirikiana na viongozi wa kimila kwa karibu sana.
Akisoma taarifa ya baraza la viongozi wa koo za maa na rika za Marya katibu wa baraza bwana Amani Lukumay, amesema eneo hilo limekuwa likitumika kwa sala na vikao vya maamuzi vya kujenga mila na desturi zao.
Na mnamo mwaka 2005 waliambiwa na serikali kusimamisha huduma hizo kwani eneo hilo limekuwa likitumika katika makazi ya watumishi wa chuo cha ufundi.
Hivyo wanaiomba serikali kutatua mgogoro huo kwani umekuwa niwa mda mrefu sana na kusababisha shughuli zao za kimila kukwama.
Mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel Fabian Daqarro, amewapongeza wamasai kwa kushikiria mila na desturi zao kwa mda mrefu.
Nae Mkuu wa wilaya ya Monduli Idd Kimanta akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, amesema kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Mkoa yamechangiwa na viongozi hao kwa kuonesha ushirikiano mkubwa kwa serikali.
Kwa upande wa serikali itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega katika maswala mbalimbali ya kujenga mkoa na nchi kwa ujumla.
Baraza la viongozi wa koo za maa na rika za marya lilikuwa likifanya vikao vyake mara kwa mara katika eneo hilo linaloita Oreteti Loongaika katika jiji la Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.