Na Mwandishi wetu
Serikali imewaagiza waajiri wa Sekta zote nchini, kuhakikisha wataalam wanaofanya kazi za Ununuzi na Ugavi wanakuwa na sifa sitahiki, kama ilivyoainishwa kwenye Sheria Na. 23 ya mwaka 2007 iliyoanzisha Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), pamoja na miongozo inayotolewa.
Maagizo hayo yametolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akifungua Kongamano la 14 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi linalofanyika kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC) mkoani Arusha na kusisitiza watalaam wa Ununuzi na Ugavi kuhakikisha wanasajiliwa na Bodi ya (PSPTB), kama inavyoelekezwa.
Dkt. Nchemba ameweka wazi kuwa, wapo watalam wa fani hiyo, wanaofanya kazi kwenye taasisi za serikali bila kusajiliwa na Bodi ya (PSPTB), jambo ambalo linasikitisha kwa kuwa tayari lipo takwa la kisheria katika kifungu cha 11 cha Sheria ya PSPTB, linaloanisha sifa stahiki za Afisa Ununuzi na Ugavi.
“Changamoto ya kuwapo kwa wataalam ambao wanafanyakazi pasipo sifa stahiki kwa sehemu kubwa inachangiwa na waajiri kuruhusu kazi za ununuzi kufanywa na waajiriwa nje ya taaluma ya ununuzi na ugavi ambayo kwa ukubwa wake inazigusa Ofisi ya Rais TAMISEMI yenye watumishi wengi zaidi wa kada hii, Ofisi ya Rais Utumishi ambao wanasimamia masuala ya ajira pamoja na Wizara Fedha kama mlezi wa kada ya ununuzi na ugavi”, alieleza Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alimwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kushirikiana na Bodi ya PSPTB, kukutana na Katibu Mkuu TAMISEMI, Katibu Mkuu Utumishi kwa utatuzi wa changamoto hiyo ili kuhakikisha kazi za ununuzi na ugavi zinafanywa na wataalamu wenye sifa na waliosajiliwa na Bodi kwa mujibu wa Sheria ya PSPTB. na sio vinginevyo.
Aidha, Dkt. Nchemba alimwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kuangalia uwezekano wa kuisaidia PSPTB kupata fedha ili iweze kufanikisha majukumu ya utekelezaji wa baadhi ya majukumu yake kisheria ikiwa pamoja na kufanya ukaguzi wa wataalam wake nchi nzima katika sekta ya umma na sekta binafsi.
Vile vile Bodi hiyo iweze kuwajengea uwezo wataalam na wadau kwenye mnyororo wa ununuzi na ugavi na kufanya utafiti wa kitaaluma unawoweza kuleta ufumbuzi wa usimamizi bora wa mnyororo wa ununuzi na ugavi mambo ambayo hayafanyiki ipasavyo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.
Kongamano hilo la 14 litafanyika kwa siku tatu likiwa na Kauli mbiu ya "Mabadiliko ya kidigitali katika kuboresha usimamizi wa mnyororo wa manunuzi na ugavi kwa maendeleo Endelevu"
#arushafursalukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.