Na Elinipa Lupembe
Halmashauri za mkoa wa Arusha, zimetakiwa kushirikiana na wadau katika kutekeleza Program Jumuishi ya Taifa ya Malezi na Makuzi na Maendeleo ya Mtoto, programu iliyozinduliwa nchini mwaka 2022.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Albano Musa, wakati akifungua Kikako cha Tathmni ya Utekelezaji wa programu hiyo, kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Amesema kuwa, ingawa mkoa unatekeleza programu hiyo, lakini ili kuongeza nguvu na kufikia malengo yaliyoainishwa ni vema kuwashirikisha wadau wote katika utekelezaji wa programu hiyo Jumuishi.
Ameweka wazi, inapofanyika tathimni na kubaini maeneo ambayo yana changamoto kubwa, washirikishwe wadau ili kuhakikisha makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto yanasimamiwa vyema kuanzia hatua za awali za ukuaji wa mtoto.
"Kila mtu anatambua thamani ya malezi ya mtoto pamoja na changamoto zinazowakabili katika hatua za makuzi, ikiwemo lishe, afya ya uzazi na uzazi salama, afya ya makuzi pamoja na fursa za mtoto katika kujifunza, bila usimamizi imara mtoto anaweza kuathirika lakini zaidi nguvu kazi ya Taifa itatetereka" Amesema Missaile
Aidha, amewaelekeza watalamu na wadau kwamba, kikao hicho kikawe dira ya kazi zinazokwenda kufanyika kwa kuangalia yaliyofanyika tangu kuzinduliwa kwa programu hiyo huku akiwasisitiza watalamu wa sekta mtambuka kufanya kazi kwa kushirikiana kama timu, kwa kuweka kipaumbe cha malezi ya mtoto, kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali kupitia programu hiyo yanafikiwa.
Naya Afisa Ustawi wa Jamii, Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na makundi maalum, Mariam Luka, licha ya kuuponheza mkoa wa Arusha kwa kuanza kuetekeleza programu hiyo kwenye nhazi ya halmashauri, amesema wizara itaendelea kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha malengo yaliyoainishwa yanafikiwa kwa kutambua kuwa hatma ya mtu mzima hutengeneza utotoni.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha, Denis Kimaro, amesema kuwa, kama mkoa wanayo kaulimbiu ya mtoto kwanza inayomtanguliza mtoto ikihusisha mahitaji na maslahi yake ya msingi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.