Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella amewahasa wananchi wa Mkoa wa Arusha, kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa kama walivyotoa kwa siku ya kwanza.
Ameyasema hayo baada ya kukagua zoezi la sensa katika Jamii ya wahadzabe Wilayani Karatu.
Amesema Jamii hiyo wameitikia wito wa Mhe. Rais Samia wa kuhesabiwa watu na makazi kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa makarani wa sensa.
Zoezi la sensa linaendelea vizuri na watu wengi wameitikia wito wa kuhesabiwa.
Nae, Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Horace Kolimba amesema katika Wilaya yake walianza zoezi la kuhesabu watu usiku wa kuamkia Agosti 23 katika hoteli na kambi za wavuvi.
Amesema zoezi linaenda vizuri na wataendelea kusimamia kwa umakini zaidi hadi litakapokamilika.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu Karia Rajabu amesema katika Jamii ya wahadzabe katika kambi ya Kijiji cha Qangdend na Kijiji cha Engamaghan jumla ya kaya 50 zimehesabiwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Engamaghan bwana Idhaya Thume amemshukuru Rais Samia kwa kuwapa nyama ambayo ni chakula kwao na hiyo ikasaidia wao kuhesabiwa kwa urahisi kwani wote hawakwenda kuwinda.
Zoezi la sensa ya watu na Makazi Mkoani Arusha lilizinduliwa rasmi na Mhe.Mongella usiku wa kuamkia Agosti 23 kwa makarani kuhesabu watu katika maeneo mbalimbali ya hoteli na nyumba za kulala wageni.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.