Wakulima wa Mkoa wa Arusha wamekiri kuvutiwa na elimu kuhusu mahindi na maharage lishe yaliyofanyiwa utafiti katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Selian, kwa kuwa yatakwenda kujibu changamoto ya utapiamlo na mavuno hafifu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Wakulima hao wamekiri hayo mapema leo wakati wa maadhimisho ya Kilimo biashara yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili katika viwanja vya TARI Seliani ambapo wamesema wengi hawakuwa wakifahamu kuhusu mahindi yenye lishe ya protini.
Loveness Urio mkulima kutoka Maji ya chai amesema “tumefurahi kupata elimu hii mimi sikuwahi kusikia kuhusu mahindi lishe yenye protini sasa tunaomba elimu hii iletwe hadi vijijini ili wakulima wazalishe mahindi hayo pamoja na maharage lishe, tunataka tuyalime watoto wetu wasipate utapiamlo”.
Naye Tajiri Laizer mkulima kutoka kata ya Lemanyata ameongeza kuwa , “tunashukuru kupata elimu ya kilimo bora katika maonyesho haya, tumejifunza kuhusu mahindi na maharage lishe kwetu vyakula vinavyotumika huenda sio lishe kamili hivyo tunaoma elimu hii nasi tuweze kulima vyakula ambavyo vitatupa kinga mwilini na kuimarisha afya zetu”.
Kwa upande wake Elieshi kitomari mkulima kutoka Maji ya chai amesema kupitia maonyesho hayo ameweza kujifunza kuhusu matumizi sahihi ya mbolea pamoja na kilimo bora cha mbogamboga
Mtafiti kutoka TARI Selian,Moses Bayinga ameeleza kuwa, wakulima 450 wameshiriki maonyesho ya kilimo biashara kwa mwaka 2024 yaliyofanyika Julai 12 na 13 na wamefikiwa na teknolojia mbalimbali kutoka kampuni na taasisi 14 ambazo zinahusika na pembejeo za kilimo lengo likiwa ni kuwahimiza wakulima kutumia teknolijia bunifu za kilimo kwa ajili ya uhakika wa chakula na lishe.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Afisa Kilimo Mkoa, Danieli Loiruk ametoa wito kwa wakulima kuacha kilimo cha mazoea bali wazingatie lishe na mahitaji ya soko.
Amesema wakulima wanapaswa kuwa na mtazamo wa ujasiriamali watumie teknolojia zinazo zalishwa TARI ili zijibu tatizo la mabadiliko ya tabia nchi na lishe pamoja na kupata ushauri kutoka kwa maafisa kilimo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.