Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Arusha wametakiwa kusimamia kikamilifu suala la lishe katika maeneo yao ili kuwa na Taifa lenye watu wenye afya bora pamoja na utimamu wa akili.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Dadi Kolimba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda katika kikao cha tathmini ya lishe Mkoa wa Arusha kilichofanyika leo tarehe 14 Februari, 2024 kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Mhe. Kolimba amesema kuwa agenda ya Mheshiwa Rais ni kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na afya njema ili kuweza kusaidia kuwa na Taifa lenye watu walio salama kiafya .
"Mheshiwa Rais ameingia mkataba na wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ambapo imeenda mpaka kwa watendaji wa kata kwasababu ya usalama wa nchi yetu kuanzia usalama wa mama na mtoto kabla na baada ya kuzaliwa". Amesema.
Aidha amewaeleza wadau hao wa lishe kuangalia afua za lishe kila wilaya kuona kama zinatekelezwa ipasavyo.
Kwa upande wake Afisa lishe Mkoa wa Ausha, Dotto Milembe amesema kuwa taarifa ya utekelezaji ya viashiria vinavyosimamiwa na mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai 2024 mpaka Desemba 2025, Mkoa umetenga fedha kiasi cha shilingi Milioni 947 kwaajili ya kutekeleza afua za lishe ambapo ni sawa na shilingi 2,490.4 kwa kila mtoto.
ameongeza kuwa, tathmini ya lishe kwenye ngazi ya kata, Mkoa wa Arusha unafanya vizuri kwa kuwa mpaka sasa wameweza kuvuka lengo la Kitaifa katika suala la lishe.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Charles Mkombachepa kwa niaba ya Katibu tawala wa Mkoa wa Arusha Missalile Albano Musa amepongeza Afua za lishe kwa kuendelea kufanya vizuri na kuwataka kuendelea kushika nafasi nzuri katika masuala ya lishe kimkoa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.