Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amewataka wakuu wa wilaya hasa wageni kwenda kusimamia zoezi la uwandikishaji wanafunzi wa awali, msingi na kidato cha kwanza katika maeneo yao.
RC Mongella ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali baada ya zoezi la kuwaapisha wakuu wapya wa Wilaya ya Arusha, Arumeru na Longido.
Amesema muongozo wa kusimamia na kuhakikisha watoto wote wanaostahili kujiunga na shule upo hivyo wakasimamie bila kuwa na huruma kwa mtu.
Aidha,amewataka wakuu hao wa Wilaya wakawe viongozi wa kutafakari bila kukurupuka hiyo itawasaidia kuweza kufanyakazi kwa weredi.
Hata hivyo, amewataka wakawahudumie wananchi kwa ukaribi zaidi.
Amewasisitiza zaidi wakatunze mazingira katika maeneo yao kwa kupanda miti kila wakati ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Nae, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa (CCM) Zelothe Steven amewataka wakuu hao wa Wilaya kwenda kusimamia ilani ya CCM katika maeneo yao kwani chama ndio kinachohitaji zaidi kutoka kwao.
Pia, wakawe wanyenyekevu na watulivu kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na hiyo itawasaidia kwenda na kasi ya Rais Samia na CCM.
Kwa upande wa Viongozi wa Dini Askofu Stanley Hotay amewashauri wakuu hao wa Wilaya wakafanye kazi zao kwa hekima maana changamoto zipo katika nafasi zao.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Wilaya walioapishwa, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda amesema wataenda kulinda amani katika maeneo yao kwani Mkoa wa Arusha ni kitovu cha utalii na kuna wageni wengi.
Vilevile, watashirikiana na viongozi wote wakiwemo wa Serikali, Dini na chama ili kuleta maendeleo ya Mkoa kwa pamoja.
Wakuu wa Wilaya wapya walioapishwa Mkoa wa Arusha ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Gasper Mtahengerwa, Marko Henry Ngu'mba Mkuu wa Wilaya ya Longido, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na Mkuu wa Wilaya ya Monduli aliye hamia Suleimani Yusuf Mwenda.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.