Na Elinipa Lupembe
Jumla ya wanafunzi 45,682 wa mkoa wa Arusha, waliofaulu mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka 2023, wamepangiwa kujiunga na kidato cha kwanza, kwenye shule za Serikali kwa mwaka ujao wa masomo 2024.
Akizungumza na mwandishi wetu, ofisini kwake, Afisa Elimu Mkoa wa Arusha, Mwl. Abel Adam Mtupwa, amesema kuwa, wanafunzi wote 45,682, wavulana ni 23,042 sawa na asilimia 50.4 na wasichana 22,640 sawa na asilimia 49.5, waliofaulu mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka 2023, wamepangiwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye, shule za Serikali, kwa mwaka wa masomo unaonza rasmi tarehe 08 Januari, 2024.
Amefafanuwa kuwa, kati yao wanafunzi 45,508, wavulana ni 22,374 na wasichana 23,134, sawa na asilimia 99.6, wamepangiwa shule za kutwa, wanafunzi 81 wamepangiwa shule za bweni za kawaida, wavulana 36 na wasichana 45, wanafunzi 35 wamepangiwa shule za vipaji maalum ambapo wavulana ni 20 na wasichana ni 15, huku wanafunzi 48 wakipangiwa kujiunga na vyuo vya ufundi wavulana 47 na wasichana 11.
Hata hivyo, Mwl. Mtupwa ameeleza historia ya wanafunzi hao kwamba, waliandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2017 wakiwa wanafunzi 57,609 na hadi kufikia mwaka 2023 walikuwa wanafunzi 54, 358 sawa na 94.3%.
Ameeleza kuwa, mwaka 2023 ufaulu katika mkoa wa Arusha, umefikia 86%, kwa wanafunzi 45,682 waliofaulu kutoka idadi ya wanafunzi 53,309, wavulana 25,863 na wasichana 27,448 waliosajiliwa na kufanya mtihani, kukiwa na ongezeko la 2% ukilinganisha na ufaulu wa jumla wa mwaka uliopita wa 2022 wa asilimia 84.
Aidha amewataka wazazi kuhakikisha wanawaandaa wanafunzi kuanza shule kwa kuwa Serikali inatoa elimu bila ada, na kuwakumbusha wazazi kuwaandaa watoto wote kuanza shule kwa wakati kwa kuwapa mahitaji yao binafsi kama waraka wa elimu unavyoelekeza.
"Serikali imekwishatekeleza majukumu yake, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya madarasa, walimu na vitabu vya kiada na zaida pamoja na kutoa elimu bila ada, jukumu la wazazi ni kuwapa watoto wao mahitaji yao binafsi kama sare za shule, madaftari na kalamu, nauli za kwenda shule, pamoja na chakula cha mchana kwa wanafunzi waliopangiwa shule za kutwa kulingana na makubaliano kati ya wazazi na kamati za shule" Amewakumbusha wazazi.
Aidha amewasisitiza wazazi kuendelea kushirikiana na walimu na kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni kwa tarehe iliyopangwa na serikali sambamba na kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anaoelekwa shule na kuoata elimu ili kufikia malengo ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ikumbukwe kuwa, hii ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 79 kifungu (g) ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya sekondari kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoendelea na kidato cha kwanza, kifungu (h) Kuongeza uandikishaji wa wanafunzi katika Elimu ya Sekondari (i) kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya sekondari kwa kuongeza idadi ya shule za sekondari nchini, Ilani ambayo imetekelezwa kwa vitendo mkoani Arusha.
Bofya Kiunganishi chini kuona shule walizopangiwa
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.