Makamu wa Rais, Dkt.Philip Mpango ameagiza Wizara ya Fedha kutoa kiasi cha shilingi milioni 290 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Samunge Wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha.
Aidha ametoa rai kwa vijana wa kike na wakiume kwenda Veta kusomea fani mbalimbali ikiwemo Ufundi wa kushona nguo badala ya kuwaachia mafundi wanawake pekee kwa kuwa ni fani ambayo vijana wanaweza kujiajiri.
Dkt.Mpango ametoa agizo hilo jana katika Kata ya Samunge wilayani Ngorongoro wakati akifungua rasmi chuo cha VETA kilichojengwa wilayani humo ambapo awali ujenzi wake ulianzishwa na vijana wa kabila la wasonjo wa rika la erumeshari.
"Wizara ya fedha hakikisheni mnaleta mara Moja kiasi cha fedha shilingi milioni 290 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa chuo hiki ujenzi wake ulianzishwa na rika la Erumeshari kisha kuungwa mkono na serikali ili wanafunzi ambao wameshaanza masomo ya fani mbalimbali katika chuo hiki wasipatwe na changamoto zozote".
Katika hatua nyingine Dkt. Mpango aliwaagiza Wakala wa Barabara Mkoa wa Arusha, (TANROADS) kutengeneza barabara inayokwenda chuoni hapo kutoka barabara kuu ya lami ya Waso- Sale ili iweke mazingira mazuri ya chuo.
"Chuo hiki ni kizuri kinavutia na wananchi hawa wa jamii ya Kisonjo wameonyesha nia ya watoto wao kupata elimu ya ufundi stadi hivyo nitumie fursa hii kumwagiza meneja wa RUWASA Mkoa wa Arusha kuhakikisha maji ya uhakika yanapatikana hapa chuoni ili wanafunzi wasipatwa changamoto ya maji".
Awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Anthony Kasore alisema mwaka 2023 serikali ilitoa kiasi cha sh.Milioni 272 Kwa lengo la kumalizia kazi zote za ujenzi wa majengo ambayo hayajakamilika.
Alisema chuo hicho kimefanikiwa kudahiki wanafunzi 147 ambapo wasichana ni 68 na wavulana 79 katika fani ya umeme,ubunifu wa mavazi,ushonaji na Teknolojia ya nguo na uashi.
Lakini pia miundombinu ya barabara inahitajika kwani barabara hiyo nyakati za mvua haipitiki na kupeleka ongezeko la gharama za usafiri sanjari na uhitaji wa Nyumba za watumishi pamoja na ukosefu wa uzio unaozunguuka chuo hicho unaopelekea uvamizi wa wanyana na wananchi.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amesema eneo la Samunge ni maarufu sana kwani watu walikuwa wakienda kupata kikombe cha babu wa Loliondo.
Alisema Samunge ni eneo la kimaendeleo kutokana na mfumo wao wa kimila kwa wanarikal la erumeshari jamii ya Wasonjo kutoa mchango mkubwa wa kimaendelo na wanalima na kufuga pia.
"Nawapongeza watu wa eneo hili kwa kusimamia dhana nzima ya maendeleo,endeleeni kuleta maendeleo".
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.