Katibu tawala wa Mkoa wa Mkoa wa Arusha Richard Kwitega, amesema utapiamlo sasa basi kwa mkoa wa Arusha, kwani wakulima na walaji wa mbogamboga wameungana pamoja kwa lengo la kuhimiza ulaji mzuri wa mbogamboga.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua warsha ya siku moja ya wadau wa uzalishaji na ulaji wa mbogamboga katika halmashauri ya Jiji la Arusha,halmashauri ya Arusha na halmashauri ya Meru.
Kwitega amesema, lishe ina muunganiko wa uzalishaji na uwandaaji wa vyakula tunavyotumia kila siku katika maisha ya mwanadamu.
Hata hivyo amesema,mpango wa kutokomeza utapiamlo kwa mkoa wa Arusha umelenga hasa kwa makundi matatu maalumu; Watoto,Wagonjwa,Wanawake walio katika umri wa kuzaa na Wazee.
Kwitega amesisitiza zaidi kuwa utapiamlo unasababishwa na upungufu wa Wanga, Vitamin, Madini,Unene kupita kiasi na wathirika wakubwa ni watoto wenye umri chini ya miaka 5 na wanawake walio katika umri wa kuzaa.
Mbali na hayo amesema changamoto kubwa zinazosababisha hali ya utapiamlo kuongezeka katika Mkoa wa Arusha ni pamoja na hali ya umaskini kwa jamii,ukosefu wa elimu ya kutosha kwa jamii.
Pia utashi na uwajibikaji wa baadhi ya viongozi, wananchi kuwa tegemezi na mabadiliko ya tabia nchi.
Hivyo elimu sahihi kwa wananchi itasaidia kutokomeza kabisa tatizo la utapiamlo na kupelekea kuwa na kizazi chenye afya bora na kuweza kukuza uchumi wa nchi kwani uzalishaji nao utakuwa.
Mganga mkuu wa Mkoa Wedson Sichalwe amesema, jitihada za pamoja bado zinaitajika kati ya serikali, wadau na wananchi katika kuhakikisha utapiamlo unatokomezwa kabisa katika mkoa wa Arusha.
Sichalwe amesema kama Mkoa utaendelea kushirikiana kwa karibu sana na wadau na wakulima wa mbogamboga katika kuhakikisha elimu sahihi inawafikiwa walaji na hata wakulima wenyewe juu ya uzalishaji na ulaji wa mbogamboga.
Akisoma taarifa fupi ya mradi wa uzalishaji na ulaji mbogamboga Mratibu wa Mradi bwana Peter Bayo kutoka taasis ya ANGONET amesema, mradi huo kwa kuanzia utakuwa katika halmashauri ya Jiji la Arusha, halmashauri ya Arusha na halmshauri ya Meru.
Amesema takribani 93% ya wananchi hawatumii mbogamboga katika milo yao na hali hii kupelekea kiwango cha utapiamlo kuwa juu.
Mradi huo unatarajia kuwafikia takribani watu 1000 kila wilaya na hasa kwa wakulima wenyewe wa mbogamboga na wanafunzi katika shule za msingi kwa kuwafundisha kuanzisha vitalu vya mbogomboga katika maeneo ya shule zao.
Peter amesema, mradi huo una miezi 3 tokea kuanzishwa na takribani kata 3 za kila wilaya zitahusishwa na mradi huu na wanatarajia zaidi ya wakulima 3000 watanufaika nao.
Amesema mradi huu wa uzalishaji na ulaji wa mbogomboga utahusisha zaidi utoaji elimu sahihi ya lishe na ulaji wa mbogamboga, kuanzisha bustani za mbogamboga katika mashule,watafanya warsha mbalimbali za uhamasishaji,utayarishaji na upikaji bora wa mbogamboga.
Mradi wa uzalishaji na ulaji wa mbogamboga umeanzishwa rasmi katika Mkoa wa Arusha na taasis ya ANGONET,TAHA na RULIDE & COMECA kwa kushirikiana na serikali ya Mkoa wa Arusha ili kuimarisha hali ya lishe na kutokomeza utapiamlo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.