Na Elinipa Lupembe
Wananchi wa kijiji cha Sero kata ya Ololosukwani, wilaya ya Ngorongoro, wameiomba Serikali kusaidia kukamilisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya kata yao, mradi unaotekelezwa na serikali kupitia fedha za Mapambano dhidi ya UVIKO 19, shilingi milioni 470, ili watoto wao waeze kusoma jirani na nyumbani.
Wananchi hao licha ya kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha za ujenzi wa shule mpya ya sekondari kijijini hapo, wanasikitishwa na majengo ya shule hiyo kutokukamilika kwa muda mrefu sasa na kuiomba serikali kukamilisha ujenzi huo.
"Tunaomba serikali itukamilishie ujenzi wa shule hii, watoto wetu wanateseka, maeneo haya yana wanyama ni hatari, kwa watoto wetu kutembea umbali mrefu wanahatarisha maisha yao, tunaomba serikali kukamilisha mradi huu kwa haraka"
Ihona Turuge amesema kuwa, tunamshukuru mama Samia kwa mradi huu mkubwa umeenda kwa haraka lakini umesimama kwa muda, ameiomba serikali kuharakisha ukamilishaji wa mradi huo.
Awali mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K.Mongella, ameviagiza vyombo vya dola, kuwachulia hatua za kisheria waliokuwa wasimamizi wa mradi huo na kusababisha mifuko 860 ya saruji kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha, akiwemo Mkuu wa shule mama ya sekondari Soitsambu, Mwl. Alex Masawe na Afisa Mtendaji wa kijiji cha Sero Ally Mrisho.
Hata hivyo Mhe. Mongella amewasisitiza watalamu wote kuthamini kazi anayoifanya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kazi ambayo inalenga kutoa huduma bora kwa watanzania bila kujali tofauti zao za kiitikadi wala kiimani
"Mama Samia anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma zote za kijamii , hususani wananchi hawa wanaoishi vijijini, watumsihi wa Umma mmepewa dhamana ya kusimamia shughuli za serikali, simamieni mirafi ikamilike kwa wakati, tambueni thamani ya miradi hii kwa wananchi, atakayefanya uzembe awajibishwe mara moja, tusioneane aibu" Amesisitiza mkuu huyo wa mkoa
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji halmasahuri ya Arusha, Nassor Shemzigwa, amepokea na kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na mkuu wa mkoa na wamejipanga kuhakikisha ujenzi huo unakamilika.
"Tunatambua umuhimu wa shule hiyo kwa watoto wa Ololosokwan, watoto ambao wako kwenye mazingira hatarishi, tunajipanga kutekeleza mradi huo na kuhakikisha uzembe uliojitokeza hauto jirudia.
Ikumbukwe kuwa, mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Ibara ya 121 inahusu kuimarisha maeneo ya kutolea huduma bora kwa wananchi kifungu (f) kujenga Majengo ya utawala katika halmashauri yamejengwa ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.
#arushafursalukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.