Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Muheshimiwa Dr. Faustine Ndungulile, amesema serikali ipo katika mchakato wa kuleta mpango madhubuti wa upimaji virusi vya UKIMWI binafsi.
Aliyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha tathimini juu ya namna ya kupunguza maambukizi ya UKIMWI Tanzania kilichoandaliwa na Taasis ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR), Jijini Arusha.
Amesema mfumo huo wa upimaji binafsi unalenga kuwafikia zaidi makundi ambayo yapo kwenye mazingira hatarishi hasa ya vijana wakike na pia kutoa wigo mpana kwa wanaume pia kupima kwani bado idadi yao ni ndogo ukilinganisha na wanawake.
Pia, serikali katika kuhakikisha inatokomeza ugonjwa huo mwaka 2016 iliweka mkakati uitwao 90, 90,90 yani (asilimia 90 ya watu wanatakiwa wawe wanajitambua hali zao,asilimia 90 waanze kutumia dawa na asilimia 90 kuhakikisha wamefubaza VVU).
Aidha, kwa mkoa wa Arusha mkakati huu umeweza kufanya vizuri sana kwa asilimia 90 ya kwanza kufanikiwa kwa asilimia 76,asilimia 90 ya pili kufanikiwa kwa asilimia 98 na asilimia 90 ya tatu imefanikiwa kwa asilimia 80.
Amesema serikali inaendelea kuboresha baadhi ya huduma kama vile; kuongeza muda wa uchukuaji dawa za kupungaza makali ya UKIMWI kutoka miezi 3 hadi 6 na kutoka mafunzo kwa baadhi ya wataalamu wa afya ili kuongeza wigo wa utoaji huduma.
Sambamba na hilo katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa na serikali ifikapo 2030 na ugonjwa huo umetokomezwa kabisa,serikali itaendelea kushirikiana na Taasis zote za serikali na binafsi zilizojikita katika kutokomeza ugonjwa huo.
Nae makamu mwenyekiti wa kamati ya bunge ya huduma ya maendeleo ya jamii mhe. Juma Nkamia (MB), amezishauri taasis zote zinazoshughulika na tafiti za mapambano dhidi ya UKIMWI kuhakikisha zinatumia lugha ya Kiswahili kama lugha kuu ya mawasiliano ili jumbe ziweze kuwafikia walengwa kwa urahisi zaidi na kueleweka.
Mkurugenzi mtendaji wa Taasis ya Utafiti wa magonjwa ya bianadamu Profesa Yunus Mgaya, amesema lengo la tafiti mbalimbali zinazofanywa na NIMR ni kuhakikisha zinasaidia malengo mbalimbali ya wizara ya afya na kurekebisha sera kwa manufaa ya nchi kwa ujumla.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.